1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ghana kuanza kutumia mimea ya viini tete

27 Desemba 2013

Ghana itaanza kutumia mbegu za mimea ya kubadilishwa kutoka kwenye asili yake, maarufu kama viini tete, kufuatia serikali kukamilisha taratibu zitakazoruhusu upandaji wa mimea mbali mbali kuanza kutumia teknolojia hiyo.

https://p.dw.com/p/1Ahgf
Ghana kuanza matumizi ya mimea ya viini tete.
Ghana kuanza matumizi ya mimea ya viini tete.Picha: picture-alliance/dpa

Hata hivyo makundi ya kiraia na baadhi ya wanasiasa kutoka vyama vya upinzani yanapinga kuanza kutumika kwa mbegu hizo kwa madai ya kuwa zina madhara kwa afya.

Kunde ni miongoni mazao ya aina tatu yaliyochaguliwa kuanza kutumia viini tete, yaani zao la Pamba ,mpunga na viazi vitamu, ambayo tayari yamethibitishwa na kufanyiwa tathimini.

Wanasayansi wamechagua mazao hayo hususan zao la kunde ambalo ni muhimu kama lishe bora kwa watu wa Ghana, hasa wale wanaotoka maeneo ya Kaskazini ambapo familia nyingi vijijini hutumia zao hilo, kama chakula kikuu.

Watu 200 Afrika hutegemea kunde

Mkulima kutoka katika wilaya ya Savelugu, Kaskazini mwa Ghana, Ibrahim Amando, ambaye ni miongoni mwa takribani wakulima milioni 200 katika bara la Afrika , wanaoishi katika maeneo kame na wanaotegemea zao hilo,ameliambia shirika la habari la IPS kuwa familia yake hutegemea zao hilo kutokana na thamani yake katika lishe.

Ibrahim, hata hivyo amelalamikia kutumia gharama kubwa ya dola 60 za Marekani kwa kununua dawa za kupulizia wadudu wanaoshambulia zao la kunde, ambapo hupulizia kila wiki, ingawa anasema hupata mavuno ya hadi magunia manne ya kilo 84 kila moja, ikiwa ni kipindi kizuri cha mavuno.

Uzalishaji wa zao la kunde nchini Ghana, zao la pili tegemezi baada ya karanga, umeongezeka kwa asilimia 50 ambapo kwa mujibu wa mratibu wa miradi ya kilimo kutoka serikalini, Dakta Ibrahim Kwai Atokple, mradi huo wa kubadilisha mimea kutoka asili yake unalenga kuimarisha usalama wa chakula na kuongeza kipato kwa wakulima wadogo.

Teknolojia ya viini tete kuboresha maisha ya wakulima wadogo Ghana.
Teknolojia ya viini tete kuboresha maisha ya wakulima wadogo Ghana.Picha: picture-alliance/dpa

Dakta Atokple amesema uvumbuzi wa kutumia viini tete ulijengwa na kufanyiwa tathimini kwa pamoja na wadau kutoka sekta binafsi na serikalini kwa kushirikiana na shirika la utafiti wa chakula la Jumuiya ya Madola nchini Australia, taasisi ya teknolojia ya kilimo Afrika yenye makao yake nchini Kenya, Baraza la wanasayansi watafiti wa kilimo Ghana na mashirika mengi kutoka Nigeria na Burkina Faso.

Wapinga matumizi ya viini tete

Matumizi ya viini tete yamepingwa na baadhi ya makundi ya kiraia, ambapo kwa upande wake, Ali Musmadi Jehu-Appiah katibu wa shirika linaloshughulikia vyakula Ghana ameitaka serikali kufanya tathimini zaidi kubaini madhara yatokanayo na viini tete kabla ya kuanza kutumika rasmi kwa teknolojia hiyo.

Amesema ikiwa Afrika itashindwa kuchukua hatua za pamoja,kujadilia hali hiyo, matumizi ya viini tete yatachukua nafasi na kutawala mfumo wa mazao asili na kuwa katika hatari zaidi ya enzi za siasa za ubaguzi wa rangi, ukoloni na utumwa ambapo ametaka kukumbukwa kwa maneno ya aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Henry Kissinger kuwa “chakula ni silaha“

Nacho chama kidogo cha upinzani nchini Ghana cha -CPP- kimezungumzia hadharani kupinga juhudi za matumizi ya viini tete kwenye mazao.

Viini tete husababisha kansa?

Ernesto Yeboah, mwanachama katika kampeni ya kupinga matumizi ya viini tete Ghana amepinga kwa kusema kuwa, utafiti uliofanywa na Marekani, Umoja wa Ulaya na mataifa mengine yaliyoendelea umeonyesha kuwepo kwa uhusiano baina ya mimea inayopandwa kwa viini tete na ugonjwa wa kansa na kuleta athari wakati wa kuzaliwa.

Kauli hiyo inapingana na Afisa wa mradi huo, Dakta Prince Addae ambaye amewataka raia wa Ghana kuondoa hofu juu ya kuanza kutumika kwa viini tete hivyo kwa madai kuwa utafiti umeonyesha hakuna madhara kwa binadaamu.

Dakta Addae ameliambia shirika la habari la IPS kuwa watu wengi wanashindwa kuelewa umuhimu wa matumizi ya viini tete na kinachopaswa ni kuwaelimisha wananchi, na kwamba nchi nyingi zinatumia mazao yaliyopandwa kwa kutumia viini tete.

Zao la kunde hutegemewa na watu wanaoishi maeneo kame Afrika.
Zao la kunde hutegemewa na watu wanaoishi maeneo kame Afrika.Picha: LemonAid

Kwa upande wake, Eric Amanung Okoree, ambaye ni kaimu mkurugenzi wa Idara ya mazingira, katika wizara ya Mazingira; Sayansi na Teknolojia ya Ghana, amesema matumizi ya viini tete kwenye mimea ni muhimu hata katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, kunapokuwa na mvua kidogo.

Mwandishi: Flora Nzema/IPS

Mhariri: Mohame Abdul-Rahman