1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ghana yavunjwa moyo na Marekani

17 Juni 2014

Goli la kichwa katika dakika za mwisho mwisho lake John Brooks liliwapa Marekani ushindi uliotokana na kibarua kigumu wa magoli mawili kwa moja dhidi ya Ghana katika uwanja wa Estadio das Nunas mjini Natal

https://p.dw.com/p/1CJYN
FIFA Fußball WM 2014 USA Ghana
Picha: Reuters

Clint Dempsey alifunga goli la kasi sana na ambalo ni la tano katika historia ya Kombe la Dunia, na kuwaweka kifua mbele vijana wa kocha Jurgen Klinsmann baada ya sekunde 29.

Lakini Andre Ayew alionekana kuwapa pointi moja Waghana wakati alipofunga goli safi baada ya kuandaliwa pasi safi ya kisigino na Asamoah Gyan, wakati kukiwa kumesalia dakika nane mchezo kukamilika.

Lakini hata hivyo uzembe wa Ghana ulimpa fursa beki wa Marekani Brooks kufunga kichwa safi kutokana na mkwaju wa kona zikiwa zimesalia dakika tano mpira kumalizika. Hilo lilikuwa goli lake la kwanza la kimataifa, na likampa ushindi Jurgen Klinsmann ambaye ameadhimisha mchuano wa 50 akiwa na timu ya taifa ya Marekani.

FIFA Fußball WM 2014 USA Ghana
Andre Dede Ayew alirejesha matumaini ya Waghana kabla ya Marekani kuharibu tena karamu dakika za mwishoPicha: picture-alliance/dpa

Black Stars waliutawala mchezo kwa muda mrefu lakini mwishoni walijuta kwa kushindwa kuzitumia fursa zao za kufunga magoli, na hasa kutoka kwa gwiji wao mshambuliaji Asamoah Gyan.

Marekani sasa itacheza mchuano ujao dhidi ya Ureno, ambao walizabwa magoli manne kwa sifuri na Ujerumani, wakiwa na matumaini kuwa wanaweza kufuzu katika 16 za mwisho.

Kocha Klinsmann amesema “kuna mambo ambayo tunaweza kuimarisha lakini leo tumepata points tatu tulizozihitaji sana”. Aliongeza kuwa “Ghana ni timu nzuri na wanajua namna ya kuumiliki mchezo. Hilo lilitarajiwa”.

Kocha wa Ghana Kwesi Appiah alikanusha madai kuwa mchezo wa vijana wake ulitokana na mgomo baridi wa wachezaji lakini akakiri kuwa Black Stars bado wasubiri malipo yao kamili ya marupurupu.

Ghana ambao walifika katika robo fainali ya Kombe la Dunia nchini Afrika Kusini mwaka wa 2010, sasa wanakabiliwa na mlima mkubwa wa kuukwea ili kujiondoa katika kundi hilo ambalo lina Ujerumani, Ureno.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/Reuters
Mhariri: Mohammed AbdulRahman