1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ghasia zaidi Misri

MjahidA30 Juni 2013

Watu wawili mmoja wao akiwa na asili ya Kimarekani wameuwawa wakati waandamanaji walipovamia ofisi ya chama tawala nchini Misri cha Muslim Brotherhood, Udugu wa Kiislamu mjini Alexandria.

https://p.dw.com/p/18yOC
Ghasia Misri
Ghasia MisriPicha: Str/AFP/Getty Images

Hii imeongeza wasiwasi mkubwa kwa maandamano yaliopangwa kufanyika hapo kesho(30.06.2013)yanayonuiwa kumng'oa madarakani rais Mohammed Mursi baada ya mwaka mmoja tangu kuwapo  madarakani.

Maafisa nchini humo wamesema Mmarekani huyo aliye na umri wa miaka 21aliyekuwa akifanya kazi katika shirika la kitalii la Marekani lililoko mjini Alexandria aliuwawa alipokuwa anachukua picha za waandamanaji. 

Wakati huo huo mtu wa tatu mwengine ambaye ni muandishi  habari  raia wa Misri, aliuwawa na wengine walijeruhiwa katika shambulizi la bomu kwenye maandamano mengine mjini Port Said. Polisi nchini Misri inasema chanzo cha shambulizi hilo hadi sasa bado hakijajulikana ingawa waandamanaji wanaamini ni bomu lililolengwa katika afisi ya chama cha Waislamu walio na itikadi kali.

Waandamanaji dhidi ya rais Mursi
Waandamanaji dhidi ya rais MursiPicha: picture alliance/AP Photo

Hata hivyo  viongozi  maarufu  wa  kidini  nchini Misri wameonya juu ya kutokea vita vya wenyewe kwa wenyewe hasa baada ya ghasia za wiki iliopita ambako watu kadhaa waliuwawa na wengine walijeruhiwa.  Viongozi  hao wameunga mkono hatua ya rais Mursi ya kutaka kuzungumza na upinzani kabla ya kufanyika maandamano makubwa hapo kesho.

Mohammed Mursi atimiza mwaka mmoja madarakani

Rais wa Misri Mohammed Mursi aliye na umri wa miaka 62 na aliyechaguliwa kwa njia ya kidemokrasia kuongoza nchi hiyo hapo kesho anatimiza mwaka mmoja tangu alipoanza kazi yake.

Sasa baadhi ya raia anaowaongoza wanamtaka aondoke madarakani kwa madai kuwa ameshindwa kutimiza matakwa ya waandamanaji mwaka 2011 waliomuweka madarakani na pia kutowashughulikia wapiga kura wengine milioni 50 ambao hawakumchagua mwaka uliopita.

Maandamano ya hapo kesho yameitishwa na kundi la Tamarod vuguvugu ambalo linadai kuwa na saini milioni 15 za watu wanaomtaka rais Mursi kuondoka madarakani na kuitisha uchaguzi wa haraka. 

Rais wa Misri Mohammed Mursi
Rais wa Misri Mohammed MursiPicha: Imago

Waandamanaji wamesema haja yao sio kumtoa Mursi madarakani peke yake lakini ni kwa yeyote ambaye hatatimiza matakwa yao ya chakula, amani, haki ya kijamii na haki ya kibinaadamu.

Kwa upande wake kiongozi mkuu wa chama cha Muslim Brotherhood Mohamed al-Beltagui amesema hawatakubali kamwe mapinduzi dhidi ya Rais Mursi.

Amnesty International yatoa tamko

Msemaji wa afisi ya rais wa Marekani Patrick Ventrell amesema Marekani inaomba pande zote mbili kuwa watulivu. Ventrell amesema viongozi wa kisiasa nchini humo wana wajibu wa kuhakikisha kuwa ghasia hazitokei nchini humo.

Hata hivyo jana jioni Marekani imesema raia wake pamoja na wanadiplomasia wanaweza kuanza kuondoka Misri kwa sababu za kiusalama.

Kwa upande wake Ujerumani imemtaka rais Mohammed Mursi kufanya mabadiliko ya haraka ili kuzuia umwagikaji wa damu zaidi.

Nembo ya shirika la Amnesty International
Nembo ya shirika la Amnesty International

Tangu kuanza kwa ghasia wiki iliopita nchini Misri watu watano tayari wameuwawa huku wengine wengi wakiwa  wamejeruhiwa. Shirika la kutetea haki za binaadamu la Amnesty International limetaka vikosi vya serikali kuhakikisha kuwa hawatumii nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji na kuhakikisha maandamano yanafanyika kwa amani.

Hassiba Hadj Sahraoui naibu mkurugenzi wa shirika hilo katika Mashariki ya kati amesema ni lazima utawala uweke wazi kuwa mtu yoyote atakayeonekana kutumia nguvu kupita kiasi atakabiliwa na mkono wa sheria.

Wakati huo huo jeshi lililoshuhudia kipindi cha mpito kutoka kwa utawala wa Mubarak hadi ule wa Mursi limeonya kuingilia kati iwapo ghasia zaidi zitashuhudiwa.

Mwandishi Amina Abubakar/AFP

Mhariri Sekione Kitojo