1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

GHAZNI : Taliban watishia kuuwa mateka zaidi

1 Agosti 2007
https://p.dw.com/p/CBdD

Kundi la Taliban nchini Afghanistan limesema mateka zaidi miongoni mwa mateka 21 wa Korea Kusini wanaweza kuuwawa wakati wowote ule baada ya kumalizika kwa muda wa mwisho waliotaka kutimiziwa madai yao leo mchana bila ya kufikiwa kwa ufumbizi katika mazungumzo yao na serikali.

Taliban imetishia kuwauwa Wakorea zaidi venginevyo serikali inakubali kufikia mchana huu kuwaachilia wafungwa kadhaa wa Kitalibani kutoka magereza ya Afghanistan.Wanamgambo hao tayari wamewauwa mateka wao wawili wa Korea.

Kundi la Taliban pia limetishia kumuuwa raia mmoja wa Ujerumani wanaemshikilia.

Helikopta za jeshi la taifa la Afghanistan leo limedondosha vipeperushi katika jimbo la Ghazni ambapo Wakorea walitekwa nyara na wanashikiliwa na kuonya watu juu ya operesheni ya kijeshi inayokuja katika eneo hilo.

Vipeperushi hivyo havikusema lini na wapi operesheni hiyo itafanyika na pia haijulikani iwapo operesheni hiyo imepangwa kuwaokowa mateka hao.