1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Goma, Nigeria na Afrika kusini magazetini

27 Mei 2013

Mapigano Goma,kuzingirwa na jeshi,ngome ya wafuasi wa itikadi kali ya dini ya kiislam wa Nigeria- Maiduguri na mvutano kuhusu haki miliki ya jina la rais wa kwanza mweusi nchini Afrika Kusini Nelson Mandela magazetini

https://p.dw.com/p/18dR9
Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki Moon akilindwa na vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa mataifa,alipokuwa ziarani GomaPicha: Reuters

Tunaanzia lakini mashariki ya jamhuri ya kimedokrasia ya Kongo ambako siku tatu kabla ya katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-moon kuanza ziara yake katika nchi za maziwa makuu,mapigano yaliripuka kati ya waasi wa M23 na vikosi vya serikali.Gazeti la die Tageszeitung linazungumzia mapigano hayo katika ripoti iliyopewa kichwa cha maneno "Raia hawana kinga."Die Tageszeitung linasema baada ya miezi sita ya utulivu mapigano yameripuka upya kati ya vikosi vya serikali na waasi wa M23 huko Goma:wakimbizi hawajui wafanyeje.Hawategemei kupata msaada wowote wa Umoja wa mataifa..Ripota wa gazeti hilo la mjini Berlin anazungumzia jinsi watoto wanavyochagiza kwa vilio,wakinamama wanavyolalamika na wakinababa wakipiga makelele kwa uchungu.Mabomu yanaendelea kuporomoshwa na milio ya bunduki chapa kalashnikov ikihanikiza..Maelfu waneingia tena njiani,wengi wao hawakubeba chochote cha maana.Wanakimbilia kutafuta hifadhi katika kituo cha Umoja wa mataifa cha Munigi-Lakini lango la kituo hicho limefungwa,hakuna anaeachiwa kuingia.Kituo hicho kilichoko umbali wa kilomita nne kaskazini ya Goma kiko karibu zaidi na uwanja wa mapigano,na huko ndiko wananchi walikokuwa wakikimbilia kutafuta hifadhi ,mapigano yalipokuwa yakizuka hapo awali.Umoja wa mataifa  umekwepa kusema chochote kuhusu hali hiyo anasema ripota wa die Tageszeitung.Afisa mmoja wa umoja wa mataifa amesema tu kawaida wakinamama na watoto huruhusiwa kuingia lakini mara hii "hali ilikuwa  ya vurumai."Die Tageszeitung limekumbusha mapigano hayo yamejiri siku tatua kabla ya ziara ya katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-moon aliyeahidi kutumwa katika kipindi cha mwezi mmoja au miwili ijayo wanajeshi zaidi wa kulinda amani katika eneo la mashariki la jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo.

Boko haram washindwa nguvu Maiduguri

Nigeria Kampf gegen Boko Haram Islamisten
Vikosi vya serikali ya Nigeria katika mapambano yao dhidi ya Boko HaramPicha: Getty Images/AFP

Nigeria pia iligonga vichwa vya habari vya yale yaliyoandikwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani kuhusu bara la Afrika katika kipindi cha wiki moja iliyopita.Mojawapo ya magazeti hayo ni Frankfurter Allgemeine lililoripoti kuhusu kuzingirwa ngome ya wafuasi wa itikadi kali ya dini ya kiislam,Boko Haram na vikosi vya serikali."Sehemu kubwa ya mji wa Maiduguri,kaskazini ya Nigeria" imezingirwa.Katika mitaa kumi na mbili ya mji huo wenye wakaazi milioni moja imetangazwa sheria ya kutotoka nje kwa muda wa saa 24,limeandika gazeti la Frankfurter Allgemeine linalozungumzia pia kuhusu msako unaofanywa na wanajeshi wa serikali majumbani katika mitaa hiyo.Mawasiliano kwa njia ya simu za mkononi yamefungwa,habari pekee zinazopatikana zinatokana na mtandao.Frankfurter Allgemeine limekumbusha yote hayo chanzo chake ni mashambulio ya Boko Haram dhidi ya miji ya Baga na Bama ambako watu wasiopungua 242 waliuwawa.Rais Goodluck Jonathan aliyataja mashambulio hayo kuwa ni "tangazo la vita."Haijulikani wangapi miongoni mwa waasi wameuwawa kufuatia opereshini hizo za jeshi.Frankfurter Allgemeine limenukuu uongozi wa jeshi la Nigeria, ukisema "Boko Harama"wamevunjwa nguvu".

Haki miliki ya jina la Mandela yagombaniwa

Nelson Madela Krankenhaus
Rais mstaafu wa Afrika kusini Nelson Mandela alipokuwa hospitali hivi karibuniPicha: picture-alliance/AP

Ripoti yetu ya mwisho katika ukurasa huu wa Afrika katika magazeti ya Ujerumani wiki hii inatufikisha Afrika kusini ambako mvutano umezuka kuhusu nani ana haki ya kumrithi rais mstaafu wa Afrika kusini,Nelson Mandela.Gazeti la Handelsblatt linazungumzia kisa cha mjukuu wa Nelson Mandela,Mandla aliyekiuzia kituo cha televisheni cha Afrika kusini,haki ya kusimamia mazishi ya babu yake.Inasemekana amepokea Euro laki tatu kwa ajili hiyo.Hata watoto wake wote wawili wa kike,inasemekana hawataki kusubiri hadi afe mwanasiasa huyo anaethaminiwa kote ulimwenguni,ili wapate natija:Katika wakati ambapo Makaziwe,mwenye umri wa miaka 60 anauza mvinyo kwa kutumia jina "Nyumba ya Mandela" mdogo wake Zenani mwenye umri wa miaka 54 anauza fulana zenye picha ya  Mandela na nambari "46664" aliyokuwa nayo alipokuwa amefungwa katika kisiwa kidogo cha Robben Island karibu na Cape Twon.Hawatosheki lakini linasema gazeti la Handesblatt.Gazeti hilo la mjini Düsseldorf limelinukuu gazeti la "Star" la mjini Johannesburg likisema mabinti hao wawili wanataka kumshitaki baba yao ili ubatilishwe uamuzi alioupitisha mwaka 2004.Wakati ule Nelson Mandela,mwenye umri wa miaka 94 hivi sasa aliwapatia haki miliki ya jina lake watu watatu anaowaamini zaidi:rafiki yake wa muda mrefu ambae ni wakili George Bizos aliyemtetea Nelson Mandela katika miaka ya 60,waziri wa ujenzi Tokyo Sexwale na wakili Baily Chuene anaemwakilisha Mandela katika kadhia hii iliyozushwa na binti zake.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/All /presse

Mhariri:Mohammed Khelef