1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Gordon Brown akabidhiwa madaraka kuiongoza Uingereza

P.Martin27 Juni 2007

Enzi ya Tony Blair kama waziri mkuu wa Uingereza inamalizika.Blair alishika madaraka akinawiri, lakini heba yake ilianza kufifia baada ya Uingereza kushiriki katika vita vya Iraq.

https://p.dw.com/p/CB3I
Gordon Brown pamoja na mkewe Sarah
Gordon Brown pamoja na mkewe SarahPicha: AP

Leo Blair ndio anamkabidhi aliekuwa waziri wa fedha, Gordon Brown,madaraka ya kuiongoza Uingereza.

Gordon Brown ambae siku ya Jumapili aliidhinishwa kama kiongozi mpya wa chama cha Labour katika mkutano maalum uliofanywa mjini Manchester,amepata umaarufu wake kama mjuzi wa uchumi.Ingawa Brown alikuwa waziri wa fedha kwa takriban miaka kumi,mzaliwa huyo wa Scotland alie na miaka 56 bado ni fumbo kwa Waingereza wengi.

Kwa maoni yake siasa haihusiki na utamaduni wa umaarufu.Amesema wito wake ni huu.

“Kufanya kazi kwa bidii:kuwajibika:kuwatendea haki wenzako:kushirikiana na watu na kuwasaidia walio na shida,iwe serikali au mmojawapo serikalini.”

Mara nyingi magazeti ya Kingereza husema kuwa Gordon Brown ni mtu wa vitendo,si maneno.Si mtu wa mawazo na itikadi,bali ni myakinifu alie na uhusiano wa karibu sana na chama chake cha Labour Kwa maoni ya mtaalamu wa siasa,Anthony Giddens:

“Wapiga kura wanangojea kuona Gordon Brown atakuwa waziri mkuu wa aina gani.Huo utakuwa mtihani mkubwa kwa Brown,kwani kinyume na hapo awali alipokuwa akizungunkwa na makaratasi ya hesabu,sasa atakuwa sana hadharani.”

Hata kuhusu siasa za nje kuna masuala mengi yanayongojea majibu.Mara nyingine tena mtaalamu wa siasa Giddens:

“Hatujui atafanya nini kuhusu siasa za nje.Je ataendelea kuwa na uhusiano wa karibu pamoja na Marekani sawa na Tony Blair?Atafanyaje kuhusu vikosi vilivyo Iraq?”

Tunachojua ni kuwa Brown anaelemea Marekani na amekuwepo Marekani zaidi kulinganishwa na Blair. Mara nyingi pia,katika mawazo yake ya kiuchumi,hutupia jicho Marekani.

Barani Ulaya nako kuna mtihani unaomngojea.Lakini kitisho kikubwa kwa mrithi wa Blair ni hofu ya upinzani mkali kutoka chama cha Konsevativ kinachoibuka,tangu kuchaguliwa kwa David Cameron kama kiongozi mpya wa chama hicho cha kihafidhina.

Hata hivyo lakini akikabiliana na sera za upinzani zisizo imara,mwanademokrasia wa kisoshalisti alie na bidii na maadili imara,ana nafasi nzuri ya kupokewa vyema.Hasa miongoni mwa wale wanaotaka kuona vitendo zaidi,baada ya kuwa na miaka kadhaa ya Blair.Gordon Brown labda hatokuwa kiongozi anaependeka,lakini huaminika.