1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Guinea Bissau kufanya raundi ya pili ya uchagauzi Aprili

Abdu Said Mtullya22 Machi 2012

Raundi ya pili ya uchaguzi wa Rais inatarajiwa kufanyika mwezi ujao nchini Guinea Bissau baada ya Tume ya uchaguzi kutangaza matokeo ya raundi ya kwanza ambapo Waziri Mkuu Carlos Gomes aliongoza.

https://p.dw.com/p/14PIV
Uchaguzi wa Rais kufanyika tarehe 22 Aprili
Uchaguzi wa Rais kufanyika tarehe 22 ApriliPicha: AP

Kwa mujibu wa Tume ya taifa ya uchaguzi, ya Guinea Bissau Waziri Mkuu Carlos Gomes aliongoza katika raundi ya kwanza ya uchaguzi wa Rais. Lakini hakupata kura za kutosha ili kuweza kushinda moja kwa moja.  Sasa Waziri Mkuu Gomes atapambana na aliekuwa  Rais wa Guinea Bissau Kumba Lala  katika raundi ya pili.

Kwa mujibu wa matokea ya awali yaliyotangazwa na tume ya uchaguzi, Waziri Mkuu  Carlos Gomes Junior amepata asilimia 48. 97 ya kura na mpinzani  wake mkuu, aliyekuwa Rais Dr Kumba Lala amepata asilimia 23. 36.  Madhali hakuna aliefikia  asilimia 50 ya kura, raundi ya pili itafanyika tarehe 22 mwezi ujao.

Juu ya  uchaguzi huo Waziri Mkuu Carlos Gomes Junior amesema,"anatetea sera ya mdahalo wa kudumu kati ya vyombo vyote vya dola, kama vile baina  ya bunge na serikali, ili kudumisha utulivu nchini na kuendeleza  ustawi."

Katika uchaguzi  huo Waziri  Mkuu Carlos Gomes Junior alisimama kwa niaba ya chama cha uhuru wa Guinea na visiwa vya  Cape Verde PAIGC ambacho hapo awali kilikuwa  cha ukombozi. Bwana Carlos amesema ameridhishwa na matokea ya raundi ya kwanza na amekanusha madai  ya wizi wa kura.  Bwana Gomes ameeleza kuwa hapendelei sana kufanyika raundi ya pili ya uchaguzi lakini amesema katika demokrasia  mtu anapaswa kuyakubali  matakwa ya wananchi.

Mpinzani wake Mkuu,Rais wa hapo awali Dr. Kumba Yala aliongoza mwito wa viongozi watano wa upinzani wa kutaka matokeo ya uchaguzi uliofanyika jumapili iliyopita yabatilishwe .Dr Kumba amedai kwamba udanganyifu ulifanyika .

Lakini watazamaji kutoka Umoja wa Afrika,Jumuiya ya uchumi ya nchi za Afrika  Magharibi na kutoka nchi zinazotumia lugha ya kireno wamesema kuwa uchaguzi wa   jumapili ulikuwa huru na wa haki.

Mwandishi:Johannes Beck

Tafsiri:Mtullya  abdu

Mhariri:Josephat Charo..