1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika yagawanyika juu ya waranti dhidi ya Bashir

Abdu Said Mtullya5 Machi 2009

Waafrika wagawanyika juu ya uamuzi wa Mahakama ya kimataifa ,ICC juu ya kutoa waranti kuwezesha kukamatwa kwa rais Bashir wa Sudan.

https://p.dw.com/p/H65M
Shida zinazowakabili watu katika kambi ya wakimbizi,Darfur Njama za al Bashir?Picha: picture-alliance/ dpa

Mahakama ya Kimataifa inayopambana na uhalifu wa kivita ICC , ya mjini The Hague imepitisha uamuzi juu ya kutoa hati ya  kisheria ya kuwezesha kukamatwa kwa rais  Omar al Bashir wa Sudan.

 Mahakama hiyo inadai kuwa rais huyo ametenda uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya  ubinadamu.

Lakini Afrika imegawanyika juu ya uamuzi wa  mahakama hiyo.

Waafrika wengi wanaitilia mashaka mahakama hiyo ya kimataifa. Wanaona kuwa hadi sasa waliofikishwa mbele ya taasisi   hiyo,hasa ni waafrika.Uchunguzi unafanyika  katika nchi kadhaa za Afrika.

Rais wa tume ya Umoja wa Afrika Jean Ping amesema kuwa siyo jambo la haki kwa  mahakama ya ICC  kuwafuatilia waafrika tu. Bwana Ping amesema inaonekana kana  kwamba taasisi hiyo inafanya majaribio  barani Afrika.

Nchi 53 za Afrika kwa kauli moja zimepinga waranti wa mahakama ya kimataifa dhidi ya   rais al Bashir.Juu ya waranti huo waziri wa mambo ya nje wa Tanzania Bernand Membe  ameeleza kuwa, sasa  itakuwa vigumu kuleta mchakato endelevu  wa  amani katika jimbo   la Darfur, kwa sababu katika upande mmoja wanapelekwa wanajeshi alfu 17 wa kulinda amani katika jimbo hilo na katika upande mwingine harakati za kukamatwa rais Bashir zinasonga mbele.

Lakini katibu mkuu wa jumuiya  ya wanasheria wa Afrika Moses Adriko amesema  kuwa ,barani Afrika hakuna taasisi zinazofanya kazi  zinazoweza kushughulikia uhalifu wa kiwango kikubwa kama huo.

Bwana Adriko pia amesema kuwa haoni sababu kwa nini kiongozi yeyote wa Afrika awe na wasi wasi  ,ikiwa anafanya kazi yake  kwa kutekeleza haki za binadamu na sheria   za kimataifa nchi mwake.