1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Haki za binaadam zinavunjwa Mali

7 Juni 2013

Vikosi maalum vya jeshi la Mali vinaelekea Kidal,ngome ya mwisho ya waasi wa Tuareg huku shirika la haki za binaadam Human Rughts Watch likilaani tena madhila yanayofanywa na pande zote mbili hasimu katika eneo hilo.

https://p.dw.com/p/18ldP

Katika ripoti yake iliyochapishwa hii leo ,shirika la Human Rights Watch linasema visa vinavyofanywa na pande zote mbili: waasi wa Tuareg na wanajeshi wa serikali ni pigo kwa juhudi za kulinda haki za binaadam kaskazini ya Mali.June mosi na pili iliyopita,wanamgambo wa Tuareg wa chama cha ukombozi wa Azawad-MNLA wanaoudhibiti mji wa Kidal waliwakamata watu 100, wengi wao ni weusi wanaotokana na makabila mengine ya nchi hiyo.Mashahidi wameliambia shirika la Human Rights Watch,wanamgambo wa MNLA wamewaibia,wamewatisha na katika kadhia nyingi nyengine wamewapiga vibaya sana watu hao.

Kwa upande wao wanajeshi wa Mali wanahusishwa na visa kama hivyo vinavyokwenda kinyume na haki za binaadam ikiwa ni pamoja na mateso na kuwatendeya sivyo wanamgambo 24 pamoja na wanakijiji wa kabila la Tuareg na Bellah,katika eneo la Mopti

"Visa hivi vipya pamoja na kuripuka upya mapigano karibu na Kidal vinaonesha umuhimu wa kuheshimiwa sheria za vita na pande zote mbili na kuhakikisha wafungwa wanatendewa ipasavyo" amesema Corinne Dufka,mchunguzi wa shirika la Human Rights Watch kanda ya Afrika Magharibi.

Wakati huo huo vikosi maalum vya jeshi la Mali vinaendelea kusonga mbele kuelekea Kidal ngome ya mwisho ya waasi wanaopigania kujitenga jimbo la Azawad.Kwa mujibu wa msemaji wa jeshi la serikali ya Mali,kanali Souleyman Maiga wanajeshi wao wanajiandaa kuingia Kidal."

Hatima ya mazaungumzo ya Ouagadougou haijulikani

Intervention in Mali
Tuareg-Kämpfer MaliPicha: picture alliance / AP Photo

Nae msemaji wa MNLA,Mussa Ag Assarid anasema:"Kwa sasa tunaitaka jumuia ya kimataifa iwe shahidi wa yanayotokea.Baadhi ya vituo vyetu vimevamiwa na jeshi la Mali.Tunataraji Ufaransa itatenda haki.Kwa vyovyote vile hatutopakata mikono,tuko kwetu huku,hatutokubali,tutapigana mpaka mwisho"

Rais Macky Sall wa Senegal ametoa wito vikosi vya Mali visiingie Kidal ili kutokorofisha juhudi za amani pamoja na kuitishwa uchaguzi kama ilivyopangwa mwishoni mwa mwezi wa Julai."Nnafikiri watu wanabidi wasubiri,tuko karibu na kufikia ufumbuzi katika mazungumzo ya Ouagadougou"amesema rais Macky Sall katika mahojiano na gazeti la Ufaransa Le Figaro.

Wawakilishi wa wa serikali ya Mali na wale wa Tuareg wamepangiwa kukutana tena ijumaa hii mjini Ouagadougou katika juhudi za kuhakikisha uchaguzi mkuu unafanyika pia Kidal.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP/Reuters

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman