1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Haki za watoto hazitekelezwi Sierra Leone

13 Septemba 2011

Matukio ya ukatili dhidi ya watoto nchini Sierra Leone yanazidi kuongezeka kila uchao, licha ya kwamba nchi hiyo ni miongoni mwa mataifa yaliyosaini mikataba ya kimataifa kuwalinda watoto

https://p.dw.com/p/12YcC
Watoto wakifanyishwa kazi. Nchini Sierra Leone matatizo haya ni makubwa sana, na ni kinyume cha haki za watoto.Picha: DW

Matukio ya ukatili dhidi ya watoto nchini Sierra Leone yanazidi kuongezaka kila siku, licha ya kwamba nchi hiyo ni miongoni mwa mataifa yaliyosaini mikataba ya kimataifa juu ya haki za watoto na kupitisha sheria yake yenyewe kuhusiana na haki hizo.

Mtoto wa miaka sita anapandisha fulana yake juu na kuonyesha mistari kadha ya makovu katika mgongo wake. Ni makovu mapya kabisa kutokana na viboko alivyopata kutoka kwa mlezi wake baada ya kupoteza fedha kiasi cha Leone 500, sarafu ya Sierra Leone, ikiwa sawa na senti kumi ya dola.

Sehemu zilizoungua katika mkono wake ni kutokana na mlezi wake kuuweka mkono huo katika moto. Wakati huo alishindwa kufuata amri, na akakataa kusalim amri alipotakiwa kuchapwa viboko.

Uvimbe wenye ukubwa wa karibu inchi moja kichwani akiwa pia na kovu kubwa ni kutokana na kichwa chake kupigwa katika ukuta. Ni kitu gani alichofanya hadi kustahili adhabu kama hiyo, hana hakika.

Hafahamu ni vipi alipata uvimbe mkubwa katika juu ya jicho lake.

Kila kovu lina hadithi yake, anasema mfanyakazi wa usaidizi wa kijamii, ambaye alikuwa na kijana huyo wa kike.

Taifa hili la Afrika magharibi lenye wakaazi wapatao milioni tano bado linaendelea kurejea katika hali ya kawaida kutokana na uharibifu mkubwa wa miongo kadha ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyomalizika mwaka 2002.

Serikali ya nchi hiyo imetia saini makubaliano kadha ya kimataifa na kuidhinisha sheria yake ya ndani ya haki za watoto katika mwaka 2007. Sheria hiyo yenye umri wa miaka minne inajumuisha haki za msingi na inatoa nafasi kwa utaratibu wa kuzitekeleza.

Lakini wengi wanasema kuwa sheria hizo bado ziko katika makaratasi tu. Taasisi zenye jukumu la kutekeleza zina majumu mengi na hazina vifaa vya kutosha , wakati ambapo wale wanaotoa msaada hawawezi kumudu mahitaji yaliyopo. Tamaduni zilizopo pamoja na umasikini uliokithiri vinachangia katika ukiukaji wa haki za watoto wa Sierra Leone.

Theresa Ojong , meneja wa mpango wa Don Bosco Fambul , anasema serikali inahitaji kulichukulia suala hilo kwa makini na kutoa nafasi kwa ajili ya utetezi zaidi , kuwahamasisha watu, na watu wanahitaji kuzungumzia zaidi suala hili.

Tuna utamaduni wa ukimya katika nchi hii, amesema Ojong, ambaye shirika lake ni tawi la shirika lisilo la kiserikali la kimataifa ambalo linatoa hifadhi, ushauri na kuwapa ushauri nasaha wale ambao hawana makaazi na watoto ambao wako katika mazingira magumu nchini Sierra Leone.

Serikali inapaswa kujitokeza kwa nguvu kwasababu ni wao ambao wanatayarisha sera. Wanazungumza tu , lakini hawatekelezi.

Katika maelezo kuhusu nchi hiyo ya mwaka 2011, Amnesty International imeripoti kuwa watoto nchini Sierra Leone wanakabiliwa na ukiukaji mkubwa wa haki zao katika maeneo kadha, ikiwa ni pamoja na kazi wanazofanyishwa watoto na ukosefu wa mpango wa serikali kuliangalia mahitaji ya vijana kama waliathirika na vita pamoja na mayatima. Watoto wa mitaani hususan wanakabiliwa na matatizo makubwa ya ukiukaji wa haki za binadamu, wakiwa wana ulinzi mdogo na wakati mwingine hawana kabisa.

Serikali imeshindwa kutekeleza na kuendeleza sheria zake yenyewe na kuheshimu majukumu ya mikataba ya kimataifa ya kuwalinda watoto na kuhakikisha haki zao, limesema shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International.

Mwandishi: Sekione Kitojo / IPS.

Mhariri : Mohammed Abdul Rahman.