1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama kuongeza wanajeshi Iraq

Admin.WagnerD10 Juni 2015

Rais Barack Obama wa Marekani anatafakari uwezekano wa kutuma wanajeshi zaidi nchini Iraq, kutoa mafunzo kwa jeshi la nchi hiyo katika juhudi za kupambana na kundi la IS, linalodhibiti eneo kubwa nchini Iraq na Syria.

https://p.dw.com/p/1FeTG
Kwa wakati huu wapo wanajeshi 3000 wanaotoa mafunzo na ushauri nchini Iraq
Kwa wakati huu wapo wanajeshi 3000 wanaotoa mafunzo na ushauri nchini IraqPicha: Getty Images/J. Moore

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa maafisa wa Marekani, Rais Obama anaelekea kuidhinisha kupelekwa kwa wanajeshi wengine 500 wa Marekani nchini Iraq, kuboresha uwezo wa vikosi vya serikali ya nchi hiyo pamoja na wanamgambo wa kisuni wanaoiunga mkono. Msemaji wa Baraza la Taifa la Usalama nchini Marekani Alistair Baskey, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba zipo hatua kadhaa zinazofikiriwa, zikiwemo kuendeleza mafunzo kwa wanajeshi wa Iraq na kuwapa zana bora za kivita.

Huku hayo yakiarifiwa watu wanane waliokuwa katika ofisi za serikali katika kitongoji cha Baghdad cha Amiriyat al-Falluja wameuawa katika shambulizi la bomu lililoripuliwa na wanamgambo watatu waliokuwa wamevaa sare za jeshi. Watu wengine 17 walijeruhiwa katika shambulizi hilo, akiwemo kiongozi wa ofisi hiyo aliyeruka kupitia dirishani katika juhudi za kunusuru maisha yake.

Mmoja wa mashahidi alielezea kilichotokea. ''Baada ya sala ya jioni jana, gari iliripuka mtaani na kusababisha uharibifu mkubwa. Watu wengi wamekufa na wengine wengi wamejeruhiwa. Mripuko huo pia uliharibi jenereta.'' Amesema shahidi huyo.

Wanajeshi wa Iraq mara nyingi wameshindwa kulizuia kundi la IS kukamata maeneo nchini humo
Wanajeshi wa Iraq mara nyingi wameshindwa kulizuia kundi la IS kukamata maeneo nchini humoPicha: picture-alliance/dpa

Kundi la IS limekiri kuhusika na shambulizi hilo, likisema washambuliaji wake wameuwa watu lililowaita ''makafiri'' zaidi ya 20.

Mkakati wa Obama wapigwa kurunzi

Mpango wa Marekeni na washirika wake kutumia mashambulizi ya anga peke yake dhidi ya kundi la IS umekuwa ukitiliwa mashaka, hasa baada ya kundi hilo kuweza kusonga mbele siku za hivi karibuni, na kuikamata miji ya Ramadi nchini Iraq na Palmyira nchini Syria, licha ya mashambulizi hayo ya ndege dhidi yao.

Lakini badala ya kubadilisha mbinu katika vita hivyo, vizara ya ulinzi ya Marekani imeamua kuongeza mafunzo wa jeshi la Iraq. Msemaji wa wizara hiyo Kanali Stevene Waren, amesema wanajeshi waliopatiwa mafunzo na Marekani wamekuwa na ufanisi mkubwa kuliko ilivyotarajiwa, na hali hiyo inawafanya waamini kuwa mafunzo kwa wanajeshi wengi zaidi, yatakua hatua ambayo inajali maslahi ya kila upande.

Mkakati wa rais Obama kutumia mashambulizi ya anga peke yake umekosolewa sana
Mkakati wa rais Obama kutumia mashambulizi ya anga peke yake umekosolewa sanaPicha: picture-alliance/dpa/S. Nickel

Vituo vya mafunzo kuongezwa

Kwa wakati huu wapo wanajeshi wa Marekani wapatao 3000 ambao wanatoa mafunzo na ushauri kwa jeshi la Iraq, na kuongezwa kwa idadi hiyo kutamaanishwa pia kuongezwa kwa vituo vya mafunzo, ambavyo kwa wakati huu ni vinne nchini Iraq.

Afisa mmoja wa Marekani amesema mafunzo ya Marekani yatajikiza zaidi kwa watu wa madhehebu ya Suni. Kwa sasa wanamgambo wa kisuni wanapewa mafunzo na jeshi la taifa la Iraq, wakitarajiwa kutoa mchango mkubwa katika kuukomboa mji wa Ramadi.

Wabunge wa chama cha Republican wameukosoa sana mkakati wa rais Obama nchini Iraq, huku baadhi yao wenye msimamo mkali wakipendekeza kupelekwa kwa wanajeshi kwenye uwanja wa vita, ambao watakuwa wakiongoza mashambulizi ya mizinga na kupanua operesheni za anga.

Rais Barack Obama alikutana na waziri mkuu wa Iraq Haider al-Abadi nchini Ujerumani Jumatatu wiki hii, na kumtaka kuonyesha mafanikio yanayopatikana kutokana na msaada wa Marekani na washirika wake katika vita dhidi ya IS.

Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe/rtre

Mhariri: Mohammed Khelef