1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hakuna mshindi wa moja kwa moja kwenye uchaguzi wa Israel

Zainab Aziz Mhariri:Iddi Ssessanga
19 Septemba 2019

Waisraeli  hawana uhakika na mustakabali wa kisiasa nchini mwao, siku mbili baada ya uchaguzi ambao kwa mara nyingine, vyama viwili vikuu vya siasa havikufanikiwa kuwa na mshindi wa moja kwa moja.

https://p.dw.com/p/3PsC0
Israel Wahl 2019 | Zeitungen nach der Wahl
Picha: DW/D. Regev

Karibu asilimia 95 ya kura zilizohesabiwa chama cha Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu cha Likud kimepata viti 32 na kile cha mpinzani wake Benny Gantz cha Buluu na Nyeupe kina viti 33. Bunge la Israel lina jumla ya viti 120.

Katika matokeo ya uchaguzi huo Avigdor Lieberman wa chama cha Yisrael Beiteinu, anabakia kuwa katikati ya wagomea hao wawili wakuu na hivyo amesisitiza juu ya kuundwa serikali ya muungano lakini amesema hawezi kushiriki kwenye serikali itakayoongozwa na Benjamin Netanyahu.

Rais wa Israeli Reuven Rivlin, atashauriana katika siku zijazo na vyama vyote kabla ya kumchagua mgombea anayeamini kuwa ni bora kupewa nafasi ya kuunda serikali ya mseto thabiti.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ametoa wito kwa mpinzani wake mkuu, jenerali wa zamani Benny Gantz, kuungana naye katika kuunda serikali ya mseto. Msemaji wa Gantz, amesema hawatatoa majibu ya haraka kutokana na wito huo wa kushangaza wa bwana Netanyahu. Gantz anatarajiwa kutoa tamko baadae leo.

Kushoto: Kiongozi wa chama cha Buluu na Nyeupe Benny Gantz. Kulia: Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu
Kushoto: Kiongozi wa chama cha Buluu na Nyeupe Benny Gantz. Kulia: Waziri Mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: picture-alliance/dpa/A. Jerozolimski

Mabadiliko hayo ya mkakati yanaonyesha kwamba Netanyahu hana jinsi hasa baada ya kushindwa tena katika uchaguzi wa Jumanne, ambao umefanyika baada ya kura ambayo pia haikumpa nguvu kubwa waziri mkuu huyo wa Israel iliyofanyika mnamo mwezi Aprili, ambapo chama chake hakikupata wabunge wengi.

Netanyahu aliwahutubia wabunge wa chama chake Likud siku yaJumatano ambapo alisema amekutana na viongozi wa vyama vya mrengo wa kulia na wameahidi kushirikiana naye kuunda serikali chini ya uwongozi wake. Hakueleza lakini jinsi walivyokusudia kushughulikia suala la kutokuwa na wingi wa wawakilishi bungeni.

Bwana Netanyahu alisistiza kuwa wakati wa kampeni za uchaguzi, alipendekeza juu ya kuundwa serikali kati ya chama chake na chama cha mpinzani wake Benny Gantz kwa sababu taifa linawategemea kuonyesha mfano bora wa uwajibikaji na kwamba wanaweza kushirikiana.

Kwa upande wake Gantz amesema anatarajia kuundwa serikali ya umoja nzuri na ametoa ufafanuzi kwamba hataki kuunda serikali hiyo kwa kushirikiana na chama cha Likud kinachoongozwa na Benjamin Netanyahu, kwa sababu ya mashtaka ya rushwa dhidi yanayomkabili waziri mkuu huyo. Hata hivyo Netanyahu amekanusha kuhusika na makosa yoyote.

Vyanzo:/RTRE/DPA/AP