1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

"Hakuna sehemu isiyo na rushwa!"

Elizabeth Shoo3 Februari 2014

Umoja wa Ulaya umezindua ripoti ya juhudi za kupambana na rushwa. Ripoti hiyo ni ya kwanza kutolewa na Umoja huo na inaelezea hali katika nchi mbalimbali na kutoa ushauri wa kupambana na rushwa.

https://p.dw.com/p/1B20v
Symbolbild Korruption
Picha: picture alliance/CTK

Rushwa ni adui wa haki. Ni msemo ambao unasikika mara nyingi hasa katika nchi zinazoendelea. Lakini hata kwenye nchi zilizoendelea, rushwa bado ni tatizo sugu. Akizindua ripoti ya kwanza ya Umoja wa Ulaya juu ya kupambana na rushwa, kamishna wa mambo ya ndani wa Umoja huo Cecilia Malmström, ameweka bayana ukubwa wa tatizo hilo hapa Ulaya.

"Ripoti hii inaonyesha wazi kwamba kiwango cha rushwa kinatofautiana kati ya nchi moja na nyingine lakini inaonyesha pia kuwa rushwa inaathiri nchi zote mwanachama. Hakuna sehemu isiyo na rushwa Ulaya," amesema Malmström.

Denmark ina kiwango kidogo zaidi cha rushwa

Inakadiriwa kwamba kila mwaka rushwa inaugharimu uchumi wa Umoja wa Ulaya kiasi cha Euro billioni 120. Kiasi hicho ni sawa na bajeti ya Umoja wa Ulaya kwa mwaka mzima. Ripoti iliyozinduliwa imefanya tathmini ya hali ya rushwa katika nchi mwanachama lakini haikuishia hapo tu bali imetoa pia ushauri wa hatua za kuchukuliwa ili kutokomeza rushwa. "Sheria zilizopo hazitiliwi mkazo na vile vile bado hakuna nia ya kweli ya kutokomeza rushwa."

Kamishna wa mambo ya ndani wa Umoja wa Ulaya, Cecilia Malmström
Kamishna wa mambo ya ndani wa Umoja wa Ulaya, Cecilia MalmströmPicha: picture-alliance/dpa

Kila mwaka, shirika la kimataifa la kupambana na rushwa Transparency International, linatoa orodha ya nchi zinazofanya vizuri katika kupambana na rushwa. Nchi nyingi za Umoja wa Ulaya zinaonekaa kuwa kielelezo bora. Kwa mfano Denmark inayoongoza kwenye orodha hiyo. Ujerumani imeshika nafasi ya 12. Lakini zipo pia nchi zilizogubikwa na rushwa. Ugiriki kwa mfano iko kwenye nafasi ya 80 na hivyo, kwa mujibu wa orodha ya Transparency International, nchi za Kiafrika kama Ghana na Rwanda zimefanikiwa kudhibiti rushwa kuliko Ugiriki.

Ramani ya Transparecy International inaonyesha kiwango cha rushwa katika nchi tofauti
Ramani ya Transparecy International inaonyesha kiwango cha rushwa katika nchi tofauti

Michango ya vyama bado tatizo

Miongoni mwa maeneo ambapo rushwa imesambaa Ulaya ni katika michango kwa vyama vya siasa. Nchini Ujerumani kwa mfano, chama cha siasa lazima kiweke wazi jina la mtu au kampuni inayotoa mchango wa zaidi ya Euro 50.000. Michango iliyo chini ya kiwango hicho inaweza kutolewa kisirisiri. Kwa chama cha kisiasa kupokea mchango si sawa na kupokea rushwa lakini msemaji mmoja wa Transparency Internatioal anaelezea hatari iliyopo.

"Fedha za michango zinatoa upenyo kwa chama kupitisha maamuzi si kwa manufaa ya umma bali kwa kuwanufaisha waliotoa mchango na kwetu hii ni sawa na rushwa," msemaji Ronny Patz ameiambia DW.

Ukweli kuonekana baadaye

Transparency International imekosoa kuwa ripoti ya Umoja wa Ulaya haijagusia tatizo la rushwa katika taasisi za Umoja huo. Hivyo shirika hilo litachapisha ripoti yake Aprili mwaka huu na kuelezea tatizo la rushwa ndani ya taasisi za Umoja wa Ulaya. Hata hivyo, Transparency International imeeleza kuwa mafanikio ya ripoti hii yataonekana katika siku za usoni.

"Swali kubwa ni iwapo nchi mwanachama zitafuata ushauri uliyotolewa katika ripoti juu ya namna ya kupambana na rushwa," amesema Patz.

Zaidi ya asilimia hamsini ya raia wa Umoja wa Ulaya wamesema kwamba wanahisi rushwa inazidi kuongezeka katika nchi wanayoishi. Ripoti mpya ya Umoja wa Ulaya itakayotolewa mwaka 2016 itaonyesha iwapo Umoja huo umefanikiwa kupiga hatua na kupambana na adui adui huyu wa maendeleo.