1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali inazidi kuwa mbaya Somalia

2 Agosti 2011

Naibu katibu mkuu wa Umoja wa mataifa na mratibu wa misaada, Valerie Amos, amesema janga la njaa katika pembe ya Afrika linasambaa na huenda hivi karibuni likaenea katika maeneo sita mengine nchini Somalia

https://p.dw.com/p/129S0
Kitisho zaidi kipo kwa watoto walio na umri wa chini ya miaka 5Picha: dapd

Hii ni baada ya Umoja huo mnamo tarehe 20 mwezi uliopita, kutangaza njaa katika maeneo mawili kusini mwa Somalia, ambapo watu milioni 3.7 wanakabiliwa na njaa. Mratibu wa misaada wa Umoja wa mataifa, Valerie Amos ameonya kuwa huenda janga hilo la njaa likaenea katika maeneo mengine matano au sita ya Somalia iwapo hapatokuwa na ongezeko la misaada.

Valerie Amos UN Nothilfekoordinatorin
Valerie Amos,Naibu katibu mkuu na mratibu wa misaada ya dharura wa Umoja wa mataifaPicha: picture-alliance/dpa

Ameeleza kuwa maelfu ya wasomali tayari wamefariki huku maelfu wengine wanakabiliwa na njaa kukiwa na athari kwa eneo zima.

Amos amesema kuwa Umoja wa Afrika utafanya mkutano wa kuchangisha fedha kwa usaidizi wa Umoja wa mataifa hivi karibuni, kusaidia kuchangisha fedha kwa eneo hilo lililoathirika na ukame.

Amedokeza kuwa kwa hivi sasa, kunahitajika dola bilioni 1.4 za dharura kuokoa maisha ya watu.

Haijabainika iwapo janga hilo la njaa limeenea hadi katika nchi ya Eritrea. Serikali ya nchi hiyo imesema kuwa Eritrea imepata mvua na haijashuhudia upungufu wa chakula.

Welternährungsprogramm der UN Luftbrücke Hilfsmittel Bevölkerung Somalia
Picha: dapd

Naibu katibu mkuu huyo wa Umoja wa matiafa ameeleza kuwa Umoja huo una taarifa kidogo kutoka mji mkuu wa Eritrea, Asmara ambayo ipo chini ya vikwazo vya baraza la usalama la Umoja wa mataifa kwa kuliunga mkono kundi la waasi Al Shabaab nchini Somalia, lakini Umoja huo umepokea thibitisho kuwa nchi hiyo imeathirika na ukame.

Ripoti ya hivi karibuni ya Umoja huo imeeleza kuwa hali katika maeneo yalioathirika kwa kiwango kikubwa na jnaga hilo nchini Ethiopia na Kenya inatarajiwa kupungua kuwa katika kiwango cha janga kutoka kile cha dharura, kufikia mwishoni mwa mwaka huu.

Lakini hali Somalia imetajwa kuwa yenye kiwango kikubwa cha utapia mlo na vifo vya watoto walio na umri wa chini ya miaka mitano, pamoja na kudhoofika kwa hali za mifugo, kuendelea kupanda bei za nafaka, na mavuno ya kiwango cha chini ya wastani.

Logo der African Development Bank Group
Picha: ADB

Kwengineko hapo jana mkuu wa benki ya maendeleo Afrika, Donald Kaberuka, amelaumu janga la njaa lililopo katika pembe ya Afrika kutokana na mabadiliko ya tabia nchi na kushindwa kwa pamoja kuvimaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Somalia.

Kaberuka ameeleza kuwa jambo la muhimu hivi sasa ni kuokoa maisha lakini pia ni lazima mpango wa muda mrefu ushughulikiwe na maafisa wa serikali kujaribu kukabiliana na tatizo hilo

Ameiomba jumuiya ya kimataifa kutoa msaada kwa maeneo yalio na amani kaskazini mwa Somalia, na kukisaidia zaidi kikosi cha Umoja wa Afrika cha kulinda amani nchini humo, AMISOM.

Mwandishi: Maryam Abdalla/Rtre/Afpe
Mhariri:Abdul-Rahman,Mohammed