1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali Mashariki ya kati magazetini

21 Novemba 2012

Juhudi za kumaliza mapigano kati ya Israel na Hamas, na uwezekano wa Uturuki kupatiwa mtambo wa kinga ya makombora-Patriot ni miongoni mwa mada zilizochambuliwa zaidi na wahariri wa magazeti ya Ujerumani.

https://p.dw.com/p/16nAm
Juhudi za kidiplomasia kumaliza mapigano kati ya Israel na wapalastinaPicha: Reuters

Tuanzie lakini Mashariki ya kati na juhudi za kusitisha silaha katika ugonvi kati ya Israel na Hamas huko Gaza.Gazeti la "Hessische Niedersächsische Allgemeine" linaandika:

Mpango wa kuweka chini silaha ungekuwa mwanzo wa kuondokewa na hofu isiyokuwa na mwisho.Pande zote mbili hasimu zitafaidika na hali hiyo.Kwasababu pande hizo mbili zitasalimika na kitisho cha mashambulio ya nchi kavu ya vikosi vya Israel.Yangesababisha mapigano makali majiani,hasara isiyokadirika ya maisha na majeruhi-na sio tu miongoni mwa raia wa kipalastina,bali pia miongoni mwa wanajeshi wa Israel.Kwa mtazamo wa muda mrefu,wakaazi wa kusini mwa Israel watafaidika tu ikiwa hali yao ya maisha itarejea kuwa ya kawaida na kuondokewa na kitisho kisichokwisha .Inamaanisha Hamas na makundi mengine ya itikadi kali yanaachana na matumizi ya nguvu.Kama watakuwa tayari kufanya hivyo-ndilo suala watu wanalojiuliza.Jibu litategemea kama Israel itapunguza vizuwizi ilivyoliwekea eneo hilo la mwambao na kama ushawishi wa chama cha udugu wa kiislam nchini Misri utasaidia kuwatanabahisha wafuasi wa Hamas.

Gazeti la "Nürnberger Nachrichten" linahisi mtutu wa bunduki sio dawa.Gazeti linaendelea kuandika

Hujuma za kijeshi hazitosaidia hata kidogo kuwavunja nguvu Hamas.Matokeo ya hujuma za angani ni vifo chungu nzima vya raia wasiokuwa na hatia,majumba yaliyobomolewa na chuki zinazozidi kukuwa.Nguvu na ushawishi wa wafuasi wa itikadi kali huko Gaza,utadhoofika tu ikiwa wakaazi wa eneo hilo watapatiwa matumaini mema.Kwa wakati wote lakini ambao watakuwa wakiishi kama wafungwa,bila ya kuwa na matumaini ya mustakbal mwema na hadhi,wafuasi wa itikadi kali hawatakuwa na hofu ya kujipatia wafuasi vijana.Na Israel haitoweza kuishi kwa amani.

Raketen Abwehrsystem Patriot der Bundeswehr
Mtambo wa Patriot kutoka jeshi la Ujerumani BundeswehrPicha: picture-alliance/dpa

Mada yetu ya pili inahusu uwezekano wa Uturuki kupatiwa mtambo wa kinga dhidi ya hujuma za makombora-Patriot kutoka jumuia ya kujihami ya NATO.Ujerumani ni miongoni mwa nchi tatu za NATO zinazotengeneza mtambo huo.Gazeti la "Der neue Tag" linaandika:

Mchango mwengine wa vikosi vya jeshi la shirikisho-Bundeswehr nchi za nje,utahitaji kibali cha bunge-Bundestag.Anaetaka kuwaona wanajeshi wa Ujerumani wakiwajibika,hahitaji kujificha kwa kutumia kizingizio cha "mshikamano miongoni mwa wanachama wa NATO."Wanajeshi watakaotakiwa kuwekwa karibu na mpaka pamoja na Syria,wanahitaji kupata ufafanuzi wa bunge la Buindestag kuhusu jukumu lao.

Italien Ratingagentur Moody's stuft Kreditwürdigkeit herab
Nembo ya shirika la Moody mjini New YorkPicha: dapd

Mada ya mwisho inahusu kishindo kinachoikaba Ufaransa baada ya taasisi ya Moody inayotathmini uwezo wa nchi kulipa madeni yake kuiwekea swali la kuuliza Ufaransa.Gazeti la "Donaukurier" linaandika:

"Azma ya kufanya mageuzi pekee haitoshi.Ikiwa rais wa Ufaransa Francois Hollande hatotekeleza alichoahidi,basi masoko ya hisa yatafichua ukweli wa mambo.Riba za juu kwa mikopo nchini humo zitaifanya nchi hiyo ya pili muhimu kiuchumi barani Ulaya izidi kupalilia mgogoro wa madeni barani Ulaya.Na Ufaransa ikiyumba yumba,na pengine kufikia hadi kuhitaji msaada,hapo mradi mzima wa Euro hautasalimika.

Mhariri:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman