1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali mjini London kabla ya uchaguzi

Zainab Aziz
6 Juni 2017

Polisi nchini Uingereza wamewatambulisha watuhumiwa wawili kati ya watatu wa mashambulizi ya London. Watuhumiwa hao wanahusika na kuwauwa watu na kuwajeruhi wengine katika daraja la London

https://p.dw.com/p/2eB2i
Großbritannien - Blumen - Trauer - London Bridge
Picha: Reuters/M. Djurica

Polisi wamefahamisha kuwa  washambuliaji hao ni Khuram Shazad Butt aliyekuwa na umri wa miaka 27, raia wa Uingereza mzaliwa wa Pakistan na ambaye hapo awali ilikuwa anachunguzwa na mamlaka nchini Uingereza. Khuram Shazad Butt, jina lake lilijulikana siku ya Jumatau kuwa ni mmoja kati ya washambuliaji watatu, alikuwa anajulikana na kikosi cha kupambana na ugaidi  MI5 na hata aliwahi kushiriki katika kipindi kinachoitwa "Jihadis Next Door" ambapo alisababisha mshtuko kutokana na maoni yake ya itikadi kali na madai yake kwamba alikuwa na mawasiliano na muhubiri mmoja mwenye itikadi kali aliyeko jela. Lakini majirani zake huko Barking, Mashariki mwa London wanamkumbuka Butt kuwa ni rafiki na mtu wa familia.

Wa pili ni Rachid Redouane, ambaye alikuwa na uraia wa Libya na Morocco, alikuwa na umri wa miaka 30, lakini pia alijulikana kwa jina la Rachid Elkhdar, ambaye umri uliorodheshwa katika jina hilo ulikuwa ni miaka 25.  Mkuu wa kupambana na ugaidi nchini Uingereza Mark Rowley amesema anawahimiza watu walio na taarifa kuhusu watuhumiwa hao, wajitokeze kuelezea taarifa hizo juu ya harakati zao na maeneo waliyokuwepo katika siku au saa kabla ya mashambulizi .  Watu saba waliuwawa na wengine kadhaa walijeruhiwa katika shambulio la Jumamosi.  Watu 36 bado wapo hospitalini mjini London wakiendelea kupokea matibabu.Hamaki imetanda nchini Uingereza hadi leo hii Jumanne kuhusu vipi mmoja kati ya washambuliaji alivyoweza kuteleza na kuwatoroka walinda usalama huku waziri mkuu Theresa May akiwa chini ya shinikizo kubwa siku mbili kabla ya uchaguzi wa hapo Alhamisi tarehe 8.

Britannien Wahlen 2017 - BBC - Theresa May
Waziri mkuu wa Uingereza Theresa MayPicha: Getty Images/WPA Pool

Bendera nchini Uingereza zilipeperushwa nusu mlingoti katika majira ya saa tano asubuhi kwa ajili ya kuwakumbuka watu saba waliouawa na wale ambao walijeruhiwa katika shambulio la Jumamosi usiku kwenye maombolezo na ibada ambayo sasa yamekuwa ni mazoea magumu baada ya mashambulizi kama hayo kutokea Uingereza katika kipindi cha chini ya miezi mitatu. Wakati huo huo Polisi wamesema walifanya uvamizi mpya katika makazi huko Mashariki ya London baada ya kuwataja washambuliaji hao wawili Khuram Shazad Butt na Rachid Redouane.

Baada ya kusitisha kampeni za uchaguzi kwa muda mfupi, kampeni hizo zilianza tena kuanzia hapo jana Jumatatu na ajenda inayoongoza ni masuala ya usalama.  Waziri mkuu Theresa May ameahidi kuweka misingi imara ya kupambana na maudhui yenye msimamo mkali mitandaoni. Lakini May pia anakabiliwa na upinzani kutokana na kumbukumbu yake juu ya usalama katika kipindi cha miaka sita nyuma alipokuwa waziri wa mambo ya ndani kabla ya kuwa waziri mkuu hapo mwaka jana. Kiongozi wa upinzani Jeremy Corbyn, alipoulizwa katika mjadala wa televisheni juu ya kuunga mkono yanayoambatana na wito wa kumtaka bibi May ajiuzulu, Corbin alisema angependelea waziri mkuu afanyae hivyo.  Kwa mujibu wa Taasisi ya kujitegemea ya mafunzo ya hazina ya nchini Uingereza kati ya mwaka 2009 na 2016, idadi ya maafisa wa polisi ilipungua kwa karibu maafisa  20,000, au karibu asilimia 14.

Mwandishi: Zainab Aziz/APE/AFPE/dw.com/p/2e9VB

Mhariri:Iddi Ssessanga