1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali nchini Misri inazidi kutokota

10 Februari 2011

Serikali ya Misri bado ingali inapinga shinikizo linaloendelea kuongezeka kutoka kwa mshirika wake mkubwa Marekani na vuguguvu kubwa la wananchi, wote wakidai mageuzi ya haraka ya kisiasa.

https://p.dw.com/p/10F07
Maandamano yapamba moto CairoPicha: dapd

Waandamanaji leo wanatimiza siku ya 17 wakiwa wamepiga kambi katika uwanja wa Tahrir mjini Cairo wakidai mishahara mikubwa, mageuzi ya kisiasa na kun'gatuka madarakani kwa Rais Hosni Mubarak.

Wasi wasi unaozidi kuongezeka miongoni mwa jumuiya ya biashara na wananchi kwa jumla kuhusu taathira ya uchumi kutokana na vurugu za zaidi ya wiki mbili unazidi kuliongezea matatizo baraza la mawaziri lililochaguliwa siku 10 zilizopita na Rais Hosni Mubarak kujaribu kukabiiana na changamoto isio kifani kuwahi kukabiliwa utawala wake wa miaka 30.

Jeshi ambalo limekuwa likitowa viongozi wa Misri kwa miongo sita limeendelea kuwa katika hali ya tahadhari huku likisifiwa na waandamanaji wanaotetea demokrasia waliopiga kambi mjini Cairo.Jeshi hilo limeahidi kurudisha maisha katika hali ya kawaida na kudumisha utulivu wa kisiasa.

Joe Biden
Makamo wa rais wa Marekani Joe BidenPicha: AP

Kamati ya kisheria imekubali hapo jana kurekebisha vifungu sita vya katiba miongoni mwao ni kuweka kikomo kwa muhula wa urais na kupanua orodha ya watu wanaostahiki kugombania wadhifa huo.

Licha ya majaribio ya kuirudisha nchi katika hali ya kawaida waandamanaji wamepuuza onyo la Makamo wa Rais Omar Suleiman wa kuwepo hatari ya kutokea mapinduzi iwapo mazungumzo na makundi ya wapinzani yatashindwa kufanikiwa.

Ägypten Vizepräsident Omar Suleiman
Makamo wa rais wa Misri Omar SuleimanPicha: picture-alliance/dpa

Ikulu ya Marekani kwa mara nyengine tena hapo jana imesema mawaziri wa Misri lazima wachukue hatua zaidi kutimiza madai ya waandamanaji wanaotaka kukomeshwa mara moja kwa utawala wa kidikteta wa miaka 30 wa Mubarak na kufanyika kwa mabadiliko makubwa ya kisheria.Robert Gibbs ni msemaji wa serikali ya Marekani.

Serikali ya Mubarak imejibu kile ilichokiita majaribio ya kutaka kulazimisha matakwa ya Marekani kwa mshirika wake huyo wa Mashariki ya Kati na kusema kwamba ni hatari kufanya mageuzi ya haraka.

Waziri wa mambo ya nje Ahmed Aboul Gheit amesema ameshangazwa na kitendo cha Makamo wa Rais wa Marekani Joe Biden kuhimiza kukomeshwa mara moja kwa sheria ya hali ya hatari ambayo Mubarak amekuwa akiitumia kwa muda mrefu kuzima upinzani.

Aboul Gheit amesema unapozunguzia mageuzi ya haraka ni sawa na kutaka kuweka matakwa yako kwa nchi adhimu na rafiki mkubwa ambayo daima imekuwa na uhusiano mzuri na Marekani.

Mvutano huo mpya katika ushirika huo ambao kwa muda mrefu umekuwa ukilelewa kwa mabilioni ya dola za msaada wa Marekani unaonyesha jinsi Misri ilivyobadilika katika kipindi cha wiki mbili,jinsi hali ilivyokua sio ya uhakika tena kwa mustakbali wa Misri na mustkabali wa ushawishi wa Marekani kwa Mashariki ya Kati ambapo watawala wake wa kiimla wamekuwa wakihangaika kudhibiti ghadhabu za umma.

Waandamanaji ambao sasa wamepiga kambi katika uwanja wa Tahrir na karibu na jengo la bunge mjini Cairo hapo kesho wanapanga kuzidi kimiminika mitaani na kuelekea katika jengo la radio na televisheni.

Mwandishi: Mohamed Dahman/ AFP,RTR,dpa

Mpitiaji Yusuf Saumu