1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali nchini Pakistan

15 Oktoba 2009

<p>Hali nchini Pakistan inazidi kuwa tete baada ya mapigano baina ya wanamgambo wa Taliban na vikosi vya usalama yaliozuka leo asubuhi katika mji wa Lahore mashariki mwa Pakistan kusababisha vifo vya watu 25. </p>

https://p.dw.com/p/K6o3
Kituo cha Polisi kilichoripuliwa na bomu mjini Lahore,PakistanPicha: AP

Watu zaidi ya 20 waliokuwa na silaha walivamia shirika la kuu la uchunguzi-FIA, chuo cha mafunzo ya polisi cha Bedian na shule nyingine ya mafunzo ya polisi iliyopo huko Manawan. Afisa wa usalama, Meja Jenerali Shafqaat Ahmad, amesema hali kwa sasa iko chini ya uangalizi wa polisi na hakuna watu wanaoshikiliwa mateka. Meja Jenerali Ahmad amesema magaidi watano waliuawa katika eneo la Baidan, lakini hajaeleza idadi ya waliojeruhiwa miongoni mwa askari polisi. Aidha, magaidi wengine watatu walijiripua wenyewe. Afisa huyo amesema, wameona maiti tano zikiwa chini, ambapo kati ya hizo ni zile zilizouwawa katika mshambulio na vikosi vya usalama na wale waliojiripua wenyewe. Mkuu wa kikosi cha uokoaji, Dr. Rizwan Naseer amesema idadi ya watu waliouawa katika mashambulio yote matatu ni 25, miongoni mwao 10 wakiwa ni magaidi.

Mashambulio hayo yametokea siku chache baada ya kutokea hujuma katika makao makuu ya  Rawalpindi, kutoa sura halisi  juu ya ukubwa wa kitisho inachokabiliana nacho Pakistan kutoka kwa wanaharakati katika jimbo la Punjab ambalo ni muhimu kwa uchumi wa taifa hilo.

Serikali inasema mashambulizi mengi huandaliwa  kutoka jimbo la Waziristan na kufanywa na Wataliban, wakisaidiwa na  washirika wao kutoka makundi ya wanaharakati kutoka jimbo la Punjab.

Watu waliokuwa na silaha  walivishambulia vituo vitatu vya polisi mjini Lahore. Watu saba akiwemo mmoja wa waliokuwa na silaha waliuwawa katika makao makuu ya mkoa ya idara wa polisi wa upelelezi ya shirikisho.  Itakumbukwa mnamo mwezi Machi mwaka jana mtu mmoja aliyejitoa mhanga kwa kujiripua alilishambulia jengo hilo hilo na kuwauwa watu 21.

Mashambulizi ya Lahore yalizusha vingora kote mjini humo  kutoka magari ya  Polisi na  ya wagonjwa.

Muda mfupi kabla ya  mashambulizi hayo mjini Lahore, mtu aliyekuwa ndani ya gari moja alijiripua nje ya kituo cha polisi mjini Kohat akiwauwa watu 10.

Serikali ya Pakistan inasema hujuma kubwa ya kijeshi dhidi ya wataliban wa msimamo mkali wapatao 10.000 katika jimbo la Waziristan kusini  ni jambo linaloweza kutokea wakati wowote.

Hadi sasa hakuna kundi lolote lililodai kuhusika na hujuma hizo za leo mjini Lahore, lakini  wataliban walidai kuhusika katika shambulizi kwenye makao makuu ya  jeshi mjini Rawalpindi hivi karibuni na kula kiapo watafanya hujuma zaidi, kulipiza kisasi  kwa kuuwawa kiongozi wao Baitullah Mehsud katika hujuma  ya anga iliofanywa na ndege za Marekani mwezi Agosti.

Pakistan yenye nguvu  ya nyuklia inakabiliwa na shinikizo  la Marekani kuitaka ichukuwe hatua kali dhidi ya  wanaharakati wa Kiislamu, wakati ambao  rais wa Marekani Barack Obama akizingatia kuongeza idadi ya wanajeshi wake wanaopigana  Afghanistan.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (RTRE)

Mhariri: M.Abdul-Rahman