1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali nchini Thailand

Oumilkher Hamidou18 Mei 2010

Baraza la Senet lapendekeza kupatanisha

https://p.dw.com/p/NQjC
Wanaharakati wa mashati mekundu wamejifungia katika kambi yaoPicha: AP

Serikali ya Thailand imeikataa miito ya "mashati mekundu" ya kuweka chini silaha,katika wakati ambapo mapambano yamepungua nguvu kidogo mjini Bangkok baada ya kuhanikiza kwa muda wa siku nne.Shirika linalopigania haki za binaadam Amnesty International linailaumu serikali kufyetua risasi za kweli dhidi ya wananchi ambao hawakua na silaha.

Moshi uliotanda angani unatoa picha ya hofu iliyoko katika mji mkuu wa Thailand-Bangkok.Jengo moja la kibiashara limetiwa moto.Lakini hakuna mapigano makubwa yaliyoripotiwa katika maeneo yanayodhibitiwa na waandamanaji wa upande wa upinzani.Jumla ya watu 38 wameuwawa na karibu ya 300 kujeruhiwa kufuatia siku nne za mapigano.

Jana usiku kiongozi mmoja wa waandamanaji,Nattawut Saikur alimpigia simu afisa mmoja wa ngazi ya juu serikalini,akishauri wanajeshi waache kuwafyetulia risasi waandamanaji .

"Upuuzi mtupu" amejibu naibu waziri mkuu Suthep Thaugssuban na kuongeza kusema tunanukuu:"vikosi vya usalama havifyetui silaha dhidi ya raia...wanafanya kazi yao kuambatana na amri waliyopewa."Mwisho wa kumnukuu.

"Magaidi ndio wanaofyetua risasi,vikosi vya usalama vinafanya hivyo ili kujihami tuu" amesema naibu waziri mkuu aliyesisitiza mkakati wa serikali wa kulizingira eneo linalodhibitiwa na waandamanaji utaendelezwa.

Flash Galerie Unruhen in Bangkok
Waandamanaji wanaendelea kukusanyika mjini Bangkok licha ya amri ya serikali ya kutawanyikaPicha: AP

Watu wasiopungua elfu tano ,wengi wao wakiwa wakinamama wamekusanyika nje ya maeneo walikopiga kambi wafuasi wa vugu vugu la mashati mekundu,licha ya amri ya kuwataka wanaharakati hao wayahame maeneo hayo.Bibi mmoja anasema

"Nimekuja kwasababu watu wengi wameshakufa hadi sasa.Nnataka serikali iache tena.Wote hawa ni binaadam na maisha yao yanabidi yathaminiwe.Nimechoka kuona picha kama hizi katika televisheni au kusoma magazetini.Hali hii lazma isitishwe tena."

Baraza la Senet la Thailand limependekeza kupatanisha ugonvi kati ya serikali na wapinzani.Kiongozi mmojawapo wa upande wa upinzani wa Mashati mekundu Nattawut Saikua amesema katika mkutano na waandishi habari wanaunga mkono pendekezo hilo ili kuepusha balaa la damau kuzidi kumwagika.

Wakati huo huo shirika linalopigania haki za binaadam limelilaumu jeshi kutumia risasi za kweli dhidi ya wananchi wasiokua na silaha."Mashahidi na picha za video zinaonyesha wazi wazi kwamba wanajeshi wamewafyetulia risasi watu ambao hawajakua na silaha na hawakuwa kitisho hata kidogo kwao" amelalamika Benjamin Zawacki,ambae ni mshauri wa masuala ya Thailand katika shirika hilo la Amnesty International.Lawama kama hizo zilitolewa pia hapo awali na shirika la Human Rights Watch .

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/afp,reuters

Imepitiwa na :Abdul Rahman