1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali ni shuari nchini Kenya lakini wajerumani wawili wanazuiliwa na polisi

Josephat Charo19 Januari 2008

Hali ya kawaida imerejea nchini Kenya baada ya maandamano ya siku tatu

https://p.dw.com/p/Cudo
Polisi nchini Kenya wakipita karibu na moto uliowashwa na wafuasi wa upinzani mjini Eldoret.Picha: AP

Wanaume wawili wajerumani, Gerd Uwe Haut na Andrej Hermlin,na mwanamke mmoja raia wa Uholanzi, Fleur Van Dissel, walioingia nchini Kenya kama waandishi wa habari wanaendelea kuzuiliwa na polisi kwa tuhuma na ugaidi baada ya kupatikana na picha za maeneo muhimu nchini humo.

Ubalozi wa Ujerumani mjini Nairobi umethibitisha kukamatwa kwa wajerumani hao wawili. Balozi wa Ujerumani nchini Kenya, Walter Lindner, amesema anashirikiana na polisi kuhakikisha wanaachiwa huru haraka iwezekanavyo. Amesema kwa sasa hawezi kutoa maelezo yoyote kuhusu kesi hiyo isije akavuruga juhudi za kuwaokoa.

Msemaji wa polisi nchini Kenya, bwana Eric Kiraithe, amesema ingawa watu hao waliingia nchini humo kama waandishi wa habari, wamekuwa wakifanya mambo ya kutilia shaka. Aidha msemaji huyo amesema wanachunguza vifaa vilivyopatikana kutoka kwa washukiwa hao. Bwana Kiraithe amesema,

´Polisi sasa wanaendelea na uchunguzi kujua hatua gani ya kuchukua. Pia tunashirikiana na polisi katika nchi nyingine kupata habari zaidi kuwahusu washukiwa hawa.´

Msemaji wa chama kikuu cha upinzani nchini Kenya Orange Democratic Movement, bwana Salim Lone, amesema mholanzi Van Diessel amekuwa akitengeza filamu fupi kuhusu kiongozi wa chama hicho mheshimiwa Rail Odinga ambayo ilionyeshwa katika televisheni moja nchini Kenya kabla uchaguzi wa tarehe 27 mwezi Disemba mwaka jana.

Van Diessel alikuwa akitayarisha filamu nyingine kumhusu Raila Odinga kama mfungwa wa kisiasa anayemshutumu rais Kibaki kwa kumuibia ushindi wa uchaguzi huo. Aidha Lone amesema mjerumani Andrej Hermlin ni mwanamuziki mashuhuri.

Watu takriban 25 wameuwawa nchini Kenya kwenye maandamano ya siku tatu ya kupinga matokeo ya uchaguzi. Bwana Tom Kgwe wa tume ya kutetea haki za binadamu nchini Kenya analaani vikali mauaji hayo.

Chama cha ODM kimesisitiza kitafanya mazungumzo pamoja na upande wa rais Kibaki chini ya uenyekiti wa mpatanishi wa kimataifa. Katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan anatarajiwa kwenda Kenya Jumanne ijayo.