1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali tete Mashariki ya kati

Abdulrahman, Mohamed3 Machi 2008

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Condolezza Rice anaelekea Mashariki ya kati leo, siku chache baada ya hujuma kubwa ya wanajeshi wa Israel katika eneo la wapalestina ukanda wa Gaza. Wapalestina 117 wakiwemo wat

https://p.dw.com/p/DHHp
Kiongozi wa Wapalestina Abbas (kulia) na Waziri mkuu wa Israel Olmert. Sasa Abbas amesitisha mawasilianoPicha: AP

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Condolezza Rice anaelekea Mashariki ya kati leo, siku chache baada ya hujuma kubwa ya wanajeshi wa Israel katika eneo la wapalestina ukanda wa Gaza. Wapalestina 117 wakiwemo watoto 22 waliuwawa pamoja na wanajeshi 2 na raia mmoja wa Israel. Wakati huo huo ,maelfu ya watu wameandamana katika mji mkuu wa Syria kupinga hujuma za Israel.

Ziara ya Waziri huyo wa mambo ya nchi za nje wa Marekani katika mashariki ya kati inakuja katika wakati ambao Wapalestiana wametangaza kusitisha mazungumzo na Israel baada ya hujuma kubwa za kijeshi za Israel katika eneo la Gaza.

Ikulu ya Marekani imezitaka pande zote mbili kumaliza machafuko na matumizi ya nguvu, kutatoa nafasi ya kuanza kwa mazungumzo ya amani ya mashariki ya kati.Kwa mujibu wa ripoti tangu Jumatano wapalestina 116 waliuwawa wakiwemo watoto 22 na Israel ilipoteza wanajeshi 2 na raia mmoja.

Waziri wa ulinzi wa Israel Ehud Barak amelilaumu kundi la Hamas kuwa chanzo kutokana na hujuma za maroketi ndani ya Israel na akitetea hatua ya serikali ya Israel na kusema,"Tunatarajia alau ukanda wa Gaza ambao sasa uko mikononi mwa wapalestina wa Hamas utakua shwari, lakini imegeuka vyenginevyo. Hauwezi kukaa tu na wala siamini kuna nchi yoyote huru duniani angeruhusu hujuma za aina hiyo dhidi ya raia wake."

Kwa upande wake Rais wa wapalestina Mahmoud Abbas ambaye jana alitangaza kusitisha mawasiliano yote na Israel,amesisitiza tena nia yake ya kusimamisha mapigano na Israel, ili kunusuru maisha ya watu wa kawaida wanaoendelea kuwa wahanga wa mgogoro huo. Abbas alipoteza mamlaka ya ukanda wa Gaza baada ya hatamu kuchukuliwa kwa nguvu na chama cha Hamas.

Katika mji mkuu wa Syria-Damascus maelfu ya watu waliandamana kupinga hujuma za Israel katika ukanda wa Gaza.Waandamanaji wakipiga kelele kumlaani Waziri mkuu wa Israel Ehud Olmert na kuwataka viongozi wa kiarabu kuchukua msimamo mkali kuhusiana na uungaji mkono wa Marekani kwa Israel.

Wakati huo huo Bw Olmert akihutubia mkutano wa chama chake cha Kadima mjini Jerusalem amesema "katu hawako tayari kuonyesha aina yoyote ya uvumilifu na hatua hiyo ya kijeshi haitasita bila ya kile alichokiita kufikia malengo yao, ambayop ni kuzuwia kabisa hujuma za maroketi zinazofanywa na Hamas ndani ya Israel."

Kamati ya kimataifa ya msalaba mwekundu imetuma malori yakiwa na misaada kutoka mji mkuu wa Joradan-Amman na dhehena ya kwanza ya chakula imeanza kupakuliwa mjini Jerulasem tayari kupelekwa Gaza

Hadi sasa Bibi Rice, anasita sita kuchukua mamlaka ya kusimamia mazungumzo kati ya Israel na Wapalestina akipendelea zaidi kuwaachia wahusika, akisisitiza wapatanishi wa Marekani waliotangulia wameshindwa. Lakini wanaomkosoa wanahoji kwamba shinikizo linahitajika na pande hizo haziwezi kuachwa peke yao kufikia suluhisho, Ni jambo lisilowezekana.

Bibi Rice anatarajiwa mjini Cairo kesho kwa mazungumzo na viongozi wa Misri juu ya hali ya mambo kabla ya kuelekea Ramadhallah kukutana na viongozi wa kipalestina na baadae Jerusalem kuzungumza na wenzao wa Israel.