1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali tete ya kiusalama eneo la Turkana Kenya

Wakio Mbogo - DW Nakuru14 Mei 2018

Majambazi waliokuwa na silaha wamewaua maafisa wawili wa polisi wa akiba huko Kapedo, Turkana Mashariki

https://p.dw.com/p/2xhXr
Krieg um Land, Vieh und Fisch in Kenia
Picha: picture-alliance/dpa

Mkasa mwingine umelikumba bonde la Ufa nchini Kenya baada ya majambazi waliojiami kuwaua maafisa wawili wa polisi wa akiba huko Kapedo, Turkana Mashariki. Mkasa huu unakuja siku nne baada ya mauaji ya watu wanne, watatu wakiwa wanafunzi walioshambuliwa wakielekea shuleni katika eneo hilo. Viongozi wa kisiasa sasa wanatupiana lawana za uchochezi huku ikielezwa kuwa huenda mgogoro wa eneo hilo umebadilika kutoka wizi wa mifugo na kuhamia kwenye ugonvi wa mipaka.

Mauaji ya maafisa 21 wa polisi katika eneo la Kapedo mwezi Oktoba mwaka 2014 uliliweka eneo hili katika ramani ya ukosefu wa usalama, hali iliyofanya mahusiano kati ya jamii mbili zilizoko eneo hilo kuwa mbaya zaidi, kila jamii ikijivua lawama. Mwaka uliopita serikali kupitia wizara ya usalama wa ndani ilitekeleza oparesheni katika eneo hilo kukabiliana na mauaji na mashambulizi, lakini wakaazi wanasema bado usalama haujatangamana.

Hapo jana maafisa wawili wa polisi wa akiba walishambuliwa na kuwaua na majambazi wanaoaminika kutoka jamii ya Pokot. Shambulizi hilo lilitokea nje ya kanisa katoliki la kapedo walilokuwa wakilichunga wakati walipofumaniwa.

Kijana wa Kiturkana akilicha mifugo huku akiwa na bunduki
Kijana wa Kiturkana akilicha mifugo huku akiwa na bundukiPicha: Reuters/Goran Tomasevic

Mkasa huu unafuatia siku nne baada ya wanafunzi watatu wa shule ya upili ya Kapedo, pamoja na dereva wa gari walimokuwa wakisafiria kuwaua na majambazi waliojiami. Gladwell Cheruyiot, mwakilishi wa wanawake kaunti ya Baringo anahoji kwamba, huenda chanzo cha mizozo katika eneo hilo kimebadilika kwani tamaduni ya wizi wa mifugo haithaminiwi tena kama hapo awali.

Wanasiasa wametajwa sana kama kiini cha mizozo katika eneo la Baringo na halikuwa jambo la kushangaza wakati mbunge wa Tiati, kaunti ya Baringo, William Kamket alipomshutumu aliyekuwa mgombea wa urais Ekuru Aukot ambaye pia ni mwenyeji wa Kapedo kutoka jamii ya Turkana.

Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter, Kamket alimtusi Aukot na kumuonya dhidi ya kuwachochea watu wa kapedo. Mwakilishi wa wanawake Gladwell Cheruyiot, anashikilia kuwa, mizozo inayoshuhudiwa hivi sasa ni ya mipaka kati ya wakaazi wa Turkana na Baringo.

Kwa sasa, shule hiyo ya upili ya kapedo imefungwa kwa muda usiojulikana kufuatia matukio ya ukosefu wa usalama. Maafisa wa polisi wameimarisha doria usiku na mchana kukabiliana na majambazi hao. Ukosefu wa usalama katika eneo hili umechochewa zaidi na upatikanaji rahisi wa silaha haramu. Wakaazi wa eneo hili wanasema wanahofia maisha yao, wasijue ni lini watapoteza maisha yao kwa risasi.

Mwandishi: Wakio Mbogo - DW Nakuru

Mhariri: Iddi Ssessanga