1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya Maldives yatangaza hali ya hatari

6 Novemba 2015

Marekani, shirika la Kimataifa la kutetea haki za binadamu na chama kikuu cha upinzani wameikosoa hatua ya kutangazwa hali ya hatari iliyochukuliwa na serikali ya Maldives zikisema ni hali inayotia wasiwasi mkubwa

https://p.dw.com/p/1H1Iy
Mji mkuu wa kisiwa cha Maldives,Male
Mji mkuu wa kisiwa cha Maldives,MalePicha: imago/Westend61

Marekani, shirika la Kimataifa la kutetea haki za binadamu na chama kikuu cha upinzani wameikosoa hatua ya kutangazwa hali ya hatari iliyochukuliwa na serikali ya Maldives zikisema ni hali inayotia wasiwasi unaoweza kusababisha vuguvugu jipya la upinzani na uhasama mkubwa nchini humo. Hali ya hatari ilitangazwa Jumatano kufuatia mripuko uliotokea katika boti ya rais pamoja na kugundulika kwa bomu na silaha .

Hatua hiyo imewapa nguvu vikosi vya usalama na jeshi kuingia na kufanya msako katika makaazi ya watu bila ya kuwa na warranti au kibali maalum na pia kuwapa uwezo wa kuwakamata watu.Maandamano,migomo pamoja na safari za raia wa nchi hiyo katika maeneo mengine ni mambo yaliyopigwa marufuku katika kipindi cha hali ya hatari cha siku 30.

Rais wa Maldive Abdulla Yameen aliyetangaza hali ya hatari
Rais wa Maldive Abdulla Yameen aliyetangaza hali ya hatariPicha: Imago/Xinhua

Maldives imekuwa katika hali ya tete na ya wasiwasi tangu Septemba 28 ulipotokea mripuko katika boti la kasi la rais wa visiwa hivyo tukio lililoandamana na hatua ya kamatakamata ya watu ikiwemo makamu wa rais Ahmed Adeeb kwa tuhuma za kushukiwa kuhusika na mripuko huo.

Rais Yameen Abdul Gayoom hakudhurika katika tukio hilo la mripuko ambalo serikali imelitaja kama jaribio la kutaka kumuangamiza rais huyo.Shirika la upelelezi la Marekani FBI ambalo limehusika kuchunguza tukio hilo limesema halikugundua ushahidi wowote kwamba mripuko huo ulisababishwa na bomu. Jeshi la nchini humo siku ya Jumatatu wiki hii lilisema limegundua bomu la kutengenezwa kwa mkono katika gari lililoegeshwa karibu na makaazi rasmi ya rais.

Siku kadhaa kabla ya hapo ghala la silaha liligunduliwa katika kisiwa ambacho kinaendelezwa kama eneo la kitalii. Kutangazwa hali ya hatari visiwani humo ni hatua iliyosababisha kuvurugika kwa mipango ya chama kikuu cha upinzani cha Maldivian Democratic ya kufanya mikutano ya hadhara siku ya Ijumaa ya kudai kuachiwa kwa kiongozi wake aliyefungwa ambaye ni rais wa zamani wa nchi hiyo Mohammed Nasheed.

Rais wa Maldive Abdulla Yameen aliyetangaza hali ya hatari
Rais wa Maldive Abdulla Yameen aliyetangaza hali ya hatariPicha: picture-alliance/AP Photo/S. Hussain

Chama hicho kimemtaka rais wa sasa Yameen Abdul Gayoom ajiuzulu madarakani kikisema amepoteza udhibiti wa nchi hiyo.Msemaji wa chama cha upinzani,Hamid Abdul Gafoor amesema rais Yammen amewatia jela au kuwapa vitisho viongozi wote wa upinzani wakati akiwawekea kesi za uhalifu wanaharakati 1,700 wa upinzani,na sasa amewageukiwa watu walioko ndani ya chama chake mwenyewe kwa kumfunga makamu wake wa rais.

Vitendo na matukio ya hivi karibuni yameifanya Mareakani kuzungumzia wasiwasi wake ambapo imeitaka serikali ya Maldive kurudisha haraka utawala wa katiba na uhuru kwa wanachi wake kwa kuifuta amri ya hali ya hatari.Shirika la haki za binadamu la Amnesty International visiwani humo limesema tangazo la hali ya hatari ni la kushtukiza na serikali haikutoa sababu za wazi kuhalalisha hatua yake ambayo inakiuka haki nyingi ikiwemo uhuru wa watu kukusanyika.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri:Daniel Gakuba