1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali ya hatari yatangazwa Pakistan

P.Martin4 Novemba 2007

Rais wa Pakistan,Pervez Musharraf ametangaza hali ya hatari katika nchi yake.Akitetea hatua hiyo amesema,anajibu tishio la wanamgambo linalozidi kuwa kubwa na vile vile serikali inashindwa kufanya kazi kwa sababu mahakama inaingilia kati.

https://p.dw.com/p/C77H
Rais wa Pakistan,Jemadari Pervez Musharraf
Rais wa Pakistan,Jemadari Pervez MusharrafPicha: AP

Katiba ya nchi imeahirishwa na askari polisi wamezingira jengo la Mahakamu Kuu mjini Islamabad na Jaji Mkuu Ifitkar Chaudhry ameondoshwa kazini.Mahakama Kuu ilitazamiwa kutoa hukumu yake siku ya Jumanne juu ya uhalali wa kumteua Musharraf mwezi uliopita, kugombea tena uchaguzi wa rais huku akishika madaraka ya kijeshi.

Kiongozi wa chama cha upinzani cha Pakistan PPP, Bibi Benazir Bhutto amesema,anakubaliana na Jemadari Musharraf kuwa kuna kitisho cha wafuasi wa itikadi kali kujiimarisha,lakini wasiwasi wake ni kuwa hali hiyo imezuka wakati wa utawala wa Musharraf.Anasema,ikiwa serikali haitobadilishwa basi wafuasi wa itikadi kali watajiimarisha.

Ripoti zinasema,wanasheria na wanasiasa wa upinzani wapatao kama dazeni moja wamekamatwa. Hivi sasa haijulikani kama uchaguzi wa bunge utafanywa mwezi wa Januari kama ilivyopangwa hapo awali.