1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Hali ya Kiutu yazidi kuwa mbaya nchini Yemen

17 Oktoba 2021

Hali ya kiutu nchini Yemen inazidi kuwa mbaya baada ya waasi wa Houthi kuendelea kuweka kizuizi kwenye moja ya wilaya za jimbo la Marib linaloshuhudia mapambano makali ya kuwania udhibiti wake.

https://p.dw.com/p/41mu2
Jemen | Kämpfe in Marib
Mapambano ya kuwania jimbo la Marib nchini Yemen Picha: AFPTV/AFP/Getty Images

Maafisa nchini Yemen pamoja na wafanyakazi wa mishirika ya Umoja wa Mataifa wamesema kizuizi kilichowekwa na waasi kwa zaidi ya wiki moja kimeondoa uwezekano wa kupelekwa msaada wa kiutu kwenye jimbo hilo na kiasi watu 37,000 wamekwama kwenye eneo hilo.

Katika wiki za karibuni waasi wa Houthi wanaoungwa mkono na Iran wamesonga mbele katika wilaya ya Abdiya Kusini kwenye jimbo la Marib na kuwalazimisha wanajeshi wa serikali inayotambuliwa kimataifa nchini Yemen kusalimu amri. Hayo ni kulingana na duru za kijeshi kutoka pande zote zinazohasimiana.

Waasi wa Houthi "wanatenda uhalifu dhidi ya ubinadamu" mjini Abdiya, wanazuia chakula, dawa na mahitaji mengi kuwafikia wenye uhitaji, amesema gavana wa jimbo la Marib Sheikh Sultan al-Aradah.

Mashambulizi yamezidi makali jimboni Marib

Shambulizi dhidi ya wilaya ya Abdiya ni sehemu ya kampeni pana ya kijeshi inayofanywa na waasi wa Houthi ikilenga kulikamata jimbo la Marib linalodhibitiwa na serikali na ambalo kwa muda mrefu waasi hao wanataka kuchukua udhibiti wake.

Jemen | As-Suwayda Flüchtlingslager
Mapigano yanafanya iwe vigumu msaada wa chakula na mahitaji mengine kuwafikia wanaohitaji.Picha: Ayman Atta/DW

Mnamo mwezi Februari waasi wa Houthi walizidisha mashambulizi yao hasa baada ya utawala wa rais Joe Biden wa Marekani kutangaza kusitisha uungaji mkono kwa muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia nchini Yemen.

Hata hivyo tangu wakati huo wamekabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa vikosi vya serikali na wapiganaji wa makundi ya kikabila yakisaidiwa na muungano huo wa kijeshi.

Wafanyakazi wawili wa huduma za msaada wa Umoja wa Mataifa wamesema waasi hao wamezuia msaada wowote wa kiutu kuifikia wilaya wanayoishikilia pamoja kupiga marufuku watu kutembea kwa zaidi ya wiki tatu.

Wamesema maelfu ya watu wamepoteza maeneo yao ya kuishi kutokana na mashambulizi yasiyobagua ya  mizinga na makombora yanayolenga makaazi ya watu na miundombinu ya wilaya ya Abdiya..

Mzingiro huo pia umezuia watu walijeruhiwa kusafirishwa nje ya wilaya hiyo.

Gavana atoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa kuwaadhibu waasi wa Houthi

Jemen | As-Suwayda Flüchtlingslager
Picha: Ayman Atta/DW

Siku ya Ijumaa kombora moja liliishambulia hospitali ya Ali Abdel-Mughni. Kulingana na shirika la madaktari wasio na mipaka hospitali hiyo ndiyo kituo kikuu cha kutoa huduma za dharura kwa watu wa wilaya ya Abdiya.

Waasi wa Houthi hasi sasa wamefanikiwa kuingia katikati ya wilaya hiyo lakini mapigano makali bado yanaendelea kwenye maeneo kadhaa katikati ya mashambulizi ya anga yanayofanywa na muungano wa kijeshi chini ya Saudi Arabia.

Muungano huo umesema umefanya mashambulizi kadhaa ya anga dhidi ya waasi wa Houthi yakilenga kuwazuia waasi hao kusonga mbele ndani ya wilaya hiyo.

Siku ya Jumamosi mjumbe maalum wa Marekani kwa Yemen Tim Lenderking alizungumza kwa njia ya simu na gavana wa jimbo la Marib aliyeitaka jumuiya ya kimataifa kuchukua "maamuzi magumu ya kulitangaza kundi la waasi wa Houthi kuwa la kigaidi na kufungua mashatka ya uhalifu wa kivita dhidi ya viongozi wake.

Waasi wa Houthi wapinga madai ya upande wa serikali

Jemen Konflikt mit Saudi-Arabien
Wapiganaji watiifu kwa waasi wa Houthi Picha: Mohammed Huwais/AFP/Getty Images

Mohammed Abdel-Salam ambaye ni mjumbe maalum wa kundi la waasi wa Houthi na msemaji wake amesema waasi hao wanapambana na wapiganaji wenye mafungamano na makundi ya itikadi kali ya Al Qaeda na lile linalojiita Dola la Kiislamu.

Ama kuhusu vizuizi vinavyotajwa, afisa huyo amesema milango iko wazi wilayani Abdiya lakini Umoja wa Mataifa hauna nia ya dhati ya kutafuta suluhu chini ya njia za kiutu.

Hata hivyo   Abdel-Salam hakutoa ushahidi wowote wa kuthibitisha madai yake na alipotafutwa na shirika la habari la Associated Press kwa ajili ya kutoa ufafanuzi zaidi hakupatikana.

Marekani kupitia msemaji wake wa wizara ya mambo ya kigeni Ned Price imeelani kwa matamshi makali kile imekitaja kuwa kuongezeka kwa mashambulizi na kusonga mbele kwa waasi wa Houthi kwenye jimbo la Marib.   

Price amesema hatua hiyo "imedhihirisha upuuzaji wa kiwango cha juu usalama wa raia" kwenye eneo hilo.