1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali ya Mashariki ya kati

Oumilkher Hamidou16 Februari 2009

Juhudi za kuweka chini silaha na kubadilishana wafungwa kati ya Israel na Palastina zimeshika kasi

https://p.dw.com/p/GvPr
Jee serikali ya aina gani itaingia madarakani Israel?


Makubaliano ya kubadilishana mwanajeshi wa kiisrael anaeshikiliwa na Hamas na wafungwa wa kipalastina wanaoshikiliwa nchini Israel yanakorofishwa na sharti la serikali ya Israel la kutaka kuwahamishia ng'ambo baadhi yao.Hali hii imejiri katika wakati ambapo juhudi za kuunda serikali mpya zimeshika kasi nchini Israel. 


Kwa mujibu wa gazeti la Al Ahram la Misri,mpango wa kubadilishana wafungwa umekwama kwasababu ya hatima ya wafungwa wanne wa kipalastina waliohukumiwa na mahakama ya Israel kwa kuhusika na mashambulio dhidi ya raia na kwa kumuuwa waziri mmoja wa Israel.

"Israel wanashikilia wafungwa hao wanne wasiruhusiwe tena kuishi Gaza na Ukingo wa magharibi" wakuu wa gazeti hilo wamesema.



Waziri mkuu wa mpito wa Israel Ehud Olmert alisema jana"kuachiliwa huru mwanajeshi Gillad Shalit,aliyetekwa nyara na wanamgambo wa kipalastina tangu mwaka 2006, ndio "kipa umbele cha mazungumzo yanayoendelea hivi sasa nchini Misri pamoja na Hamas .Mazungumzo hayo yamelengwa kuimarisha uamuzi wa kuweka chini silaha huko Gaza.


"Kwanza tunataka Gilad Shalid aachiwe huru,baadae biashara haramu ya silaha izuwiliwe ,na halafu silaha ziwekwe chini" amesema waziri mkuu wa mpito wa Israel alipokua akihutubia mkutano wa wakuu wa mabaraza ya wayaahudi wa kimarekani mjini Jerusalem.


Waziri mkuu wa mpito wa Israel amezungumzia uwezekano wa kuachiliwa mamia ya wafungwa wa kipalastina ili kurahisisha kuachiliwa huru mwanajeshi huyo mmoja wa Israel.Kituo kimoja cha televisheni cha Israel,kinazungumzia uwezekano wa kuachiwa huru hivi karibuni mwanasiasa masdhuhuri wa kipalastina  Marwan Barghouti anaetumikia kifungo cha maisha nchini Israel.Ripoti hiyo imezidisha uvumi huenda Gilad Schalit akaachiwa huru pia hivi karibuni.


Wakati huo huo juhudi za kuunda serikali ya vyama vingi zimeshika kasi baada ya uchaguzi mkuu wa jumanne iliyopita nchini Israel.


Waziri wa mambo ya nchi za nje Tzipi Livni amesema chama chake Kadima hakitojiunga na serikali yoyote ya muungano itakayoongozwa na kiongozi wa Likoud Benjamin Netanyahu.


Kwa mujibu wa matokeo ya uchaguzi huo wa bunge,chama cha Kadima kimejikingia viti 28 kati ya 120 vya bunge-Knesset huku chama cha Likoud kimejipatia viti 27.Benjamin Netanyahu anatazamiwa kuwa na nafasi nzuri ya kuunda serikali kwa msaada wa vyama vya mrengo wa kulia.


Mara baada ya matokeo rasmi kutangazwa jumatano ijayo,rais Shimon Peres ataanza mazungumzo na viongozi wa vyama kwa lengo la kumteuwa mmojawao anaestahiki kuunda serikali ya muungano wa vyama vingi.


Kiongozi wa utawala wa ndani wa Palastina,Mahmoud Abbas ameshasema,"hawatokubali mazungumzo ya amani pamoja na Israel yaanzie mwanzo" serikali mpya itakapoundwa.


Benjamin Netanyahu,kiongozi mkakamavu wa chama cha Likud,anapinga kuundwa taifa la Palastina lenye mamlaka kamili-mada ambayo ndio kiini cha mazungumzo ya amani kati ya Israel na Palastina yaliyoanza November mwaka 2007 mjini Annapolis nchini Marekani.