1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali ya mashariki ya kati

Oumilkher Hamidou15 Oktoba 2010

Miito ya ujenzi wa makaazi mepya ya walowezi wa kiyahudi katika Jerusalem ya mashariki inatishia kuvunja mazungumzo ya amani kati ya Israel na Palastina

https://p.dw.com/p/PfDL
Har Homa,makaazi ya wahamiaji wa kiyahudi katika eneo la Mashariki la JerusalemPicha: picture-alliance/ dpa

Israel imeanzisha upya ujenzi wa makaazi ya walowezi katika eneo la mashariki la Jerusalem bila ya kujali kitisho cha kuvunjika mazungumzo ya amani pamoja na wapalastina.Jumuia ya nchi za kiarabu imeonya itautaka Umoja wa mataifa iitambue dola ya Palastina .

Waziri wa makaazi wa Israel ametangaza mipango ya kujengwa nyumba 238 kwaajili ya wayahudi katika mitaa miwili ya Jerusalem ya Mashariki-Ramot na Pisgat Zeev.

Mkuu wa tume ya Palastina katika mazungumzo ya amani Saeb Erakat ameituhumu serikali ya waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kufanya kila liwezekanalo ili kama alivyosema: "kuuwa fursa yoyote ya kuanza upya mazungumzo" na kuitolea mwito Marekani iingilie kati kuupatia ufumbuzi mzozo wa ujenzi wa makaazi ya wayahudi katika ukingo wa magharibi.

Hii ni miito ya mwanzo ya ujenzi tangu September 26 iliyopiota,yalipomalizika marufuku ya miezi 10 ya ujenzi wa makaazi ya wahamiaji wa kiyahudi katika ardhi za wapalastina katika Ukingo wa Magharibi.

Ingawa marufuku hayo hayakulihusu eneo la mashariki la Jerusalem lililotekwa na kukaliwa na Israel tangu June mwaka 1967,hata hivyo serikali ya Israel ilijiepusha ,miezi iliyopita kutoa miito ya ujenzi katika mitaa ya wahamiaji wa kiyahudi katika mji huo.

"Tunalaani moja kwa moja uamuzi huu na tunautaka utawala wa Marekani uitwike serikali ya Israel jukumu la kuvunjika mazungumzo na utaratibu wa amani kutokana na ushupavu wake kutaka kuuwa kila nafasi ya kuanza upya mazungumzo." Amesema Saeb Erakat.

Ministerpräsidenten Benjamin Netanjahu bei Koalitionsverhandlungen in Tel Aviv
Waziri mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: AP

"Tangazo hilo ni la kisiasa na limetolewa makusudi kwa lengo la kuvuruga mazungumzo ya amani pamoja na wapalastina" amesema hayo Hagit Ofran,mwanaharakati wa vuguvugu linalopinga ujenzi wa makaazi mepya-lijiitalo "Amani sasa."

Kwa mujibu wa gazeti la Israel Yediot Aharonot,serikali ya Israel imetoa tangazo hilo la ujenzi wa makaazi mepya baada ya kuiarifu serikali ya Marekani.

Pindi suala la ujenzi wa makaazi ya wayahudi likiselelea,jumuia ya nchi za kiarabu inaweza kufikiria uwezekano wa kuutaka umoja wa mataifa uitambue dola ya Palastina na kuikubalia uanachama kamili-amesema hayo waziri wa mambo ya nchi za nje wa Misri Ahmed Abu Gheith mjini Brussels.Anasema amelizusha suala hilo jana usiku wakati wa mazungumzo pamoja na mawaziri wenzake wa Ujerumani,Ufaransa,Uengereza,Hispania na Italy.

Hali ya kukwama mazungumzo ya ana kwa ana ya amani kati ya Israel na Palastina inatishia pia kukorofisha mkutano unaotaka kuitishwa na rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa wiki ijayo, kati ya waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu,kiongozi wa utawala wa ndani wa Palastina Mahmoud Abbas na rais wa Misri Hosni Mubarak mjini Paris .

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP/Reuters

Mpitiaji:M.Abdul-Rahman.