1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali ya matumaini kwa mazungumzo ya Syria

Admin.WagnerD2 Mei 2016

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry amesema leo kwamba mazungumzo yanayofanyika mjini Geneva yanakaribia kurefusha usitishaji mapigano mjini Aleppo, mji wa kaskazini mwa Syria uliogawika.

https://p.dw.com/p/1Igdq
John Kerry Staffan de Mistura Genf Schweiz
Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry(kushoto) na Staffan de Mistura(kulia)Picha: Reuters/D.Balibouse

Mapigano nchini Syria ambako ongezeko la machafuko katika wiki za hivi karibuni yamekaribia kuvunja mazungumzo ya amani yanakaribia kupata ufumbuzi.

Kerry yuko mjini Geneva kwa ajili ya mazungumzo na maafisa wengine muhimu kujaribu kuokoa usitishaji mapigano wa kwanza mkubwa katika muda wa miaka mitano ya mapigano nchini Syria, ambayo yalifikiwa mwezi Februari kwa kuungwa mkono na Marekani na Urusi, lakini yamekaribia kuvunjika hivi karibuni.

John Kerry
John Kerry waziri wa mambo ya kigeni wa MarekaniPicha: picture alliance/AP Images/J. L. Magana

Syria imetangaza hatua za kusitisha mapigano katika maeneo mbali mbali wiki iliyopita lakini hadi sasa imeshindwa kupanua hatua hizo hadi Aleppo, ambako mashambulizi ya anga ya serikali na waasi kushambulia kwa makombora vimesababisha kuuwawa kwa raia katika muda wa wiki moja iliyopita, ikiwa ni pamoja na zaidi ya watu 50 katika hospitali ambayo waasi wanasema ilishambuliwa kwa makusudi kabisa.

Mapendekezo yajadiliwa

Mjini Geneva waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry amesema kwamba "mapendekezo kadhaa " yanajadiliwa yenye lengo la kupata njia ya kurejesha hata usitishaji wa muda wa mapigano katika nchi hiyo iliyoharibiwa kwa vita.

Genf Friedensgespräche zu Syrien - High Negotiations Committee
Wajumbe wa kamati ya juu ya majadiliano ya upinzani nchini SyriaPicha: Reuters/D. Balibouse

"Namshukuru sana Staffan de Mistura mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Syria kwa kazi yake nzuri, na juhudi zake katika mwezi mmoja uliopita kujaribu kuleta uhai katika hatua za kisiasa katikati ya mzozo ambao unaonekana umeshindikana na unakera kila mtu duniani , nadhani."

Baada ya kukutana na waziri wa mambo ya kigeni wa Saudi Arabia na mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa Staffan de Mistura, Kerry amesema anamatumaini ya kupata uwazi zaidi katika siku zijazo ama zaidi kuhusiana na kurejesha usitishaji mapigano nchi nzima. Marekani na Urusi zimekubaliana kuwabakisha maafisa zaidi mjini Geneva kushughulikia suala hilo.

Schweiz Genf Staffan de Mistura UN Syrien Vermittler
Mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Syria Staffan de MisturaPicha: Getty Images/AFP/F. Coffrini

Wito wa Ufaransa

Wakati huo huo Ufaransa imetoa wito kwa kundi la kimataifa linalounga mkono Syria kufanya mkutano wa dharura wa ngazi ya mawaziri kurejesha makubaliano hayo ya kusitisha mapigano yanayoonekana kuharibika katika njia sahihi, ikishutumu mashambulizi ya anga ya utawala wa Syria yaliyosababisha watu kuuwawa.

Ufaransa imelitaka kundi hilo la ISSG "kurejesha usitishaji mapigano" ikisisitiza haja ya kuwalinda raia, na kutoa nafasi ya majadiliano kuelekea suluhisho la kisiasa," amesema msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni Romain Nadal.

Syrien Krieg Kämpfe in Aleppo - Zerstörung Krankenhaus Ärzte ohne Grenzen
Mji wa Aleppo ulivyo hivi sasa baada ya mashambuliziPicha: Reuters/A. Ismail

Kwa upande mwingine , bomu lililokuwa katika gari liliripuka katika eneo linaloshikiliwa na waasi la Salhin mjini Aleppo, likionekana kulenga baraza la mahakama ya Kiislamu.

Mripuko huo umewajeruhi mwanasheria na watu wengine kadhaa, kwa mujibu wa kamati za eneo hilo zinazofanya uratibu, zikiwa ni mtandao wa wanaharakati.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / ape

Mhariri: Yusuf , Saumu