1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali ya wasiwasi mashariki mwa DRC kufuatia mashambulizi

Jean Noel Ba-Mweze25 Machi 2021

Hofu imetanda katika mkoa wa Ituri kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ambako bado hadi sasa vijiji kadhaa sasa vimesalia mahakame kufuatia mashambulizi kutoka kwa makundi yenye silaha.

https://p.dw.com/p/3r8yV
DRK Symbolbild FARDC
Picha: Alain Wandimoyi/AFP

Hali ya usalama bado ni ya wasiwasi katika mkoa wa Ituri kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ambako bado hadi sasa vijiji kadhaa sasa vimebaki bila wakaazi kufuatia mashambulizi yanayofanywa na vikundi mbalimbali vinavyomiliki silaha.

Sasa wakaazi wa huko wamemtaka Rais Felix Tshisekedi kuchukuwa hatua yeye binafsi za kurejesha amani mkoani humo. 

Wakaazi wa Ituri na mashariki mwa Kongo kwa ujumla wamekuwa wahanga wa ukatili unaofanywa na vikundi vyenye silaha dhidi ya raia kwa muda mrefu.

Soma zaidi: Marekani yapiga marufuku makundi mawili ya DRC na Msumbiji


Hali imezidi kuwa mbaya katika siku za hivi karibuni, ambapo tangu wiki iliyopita mashambulizi hayo yamesababisha vifo vya watu kadhaa na wengine wenginkujeruhiwa huko Ituri, ambako maelfu wameyakimbia makaazi yao, kama alivyothibisha Dieudonné Lossa Dekhana, mratibu wa shirika la kiraia ya Ituri. "Kulikuwa na mapigano kati ya wanamgambo wa Codeko na jeshi ng'ambo za Nizi. Watu waliouawa ni kumi na wawili na waliojeruhiwa kumi na nne. Watu wengi wamekimbia. Mama moja aliuwawa na askari jeshi, pia baba moja alikuwa akitoka shambani aliuwawa na wanamgambo wa FRPI. Waasi wa ADF waliuwa pia mtu moja kule na vijana wawili pia waliuawa."

Rwanda na Kongo kukutana kujadili juu ya kadhia hiyo
Miongoni mwa wanamgambo wanaosababisha ukosefu wa usalama katika maeneo hayo ya Kongo, ni vikundi vya wenyeji na vile vya wageni, wakiwemo waasi wa Rwanda na wa Uganda.

Rwanda na Kongo zinatarajia hivi karibuni kuwa na mkakati wa pamoja kama ilivyokubaliwa wiki iliyopita, katika mkutano uliowakutanisha hapa Kinshasa, wataalamu wa usalama kutoka nchi hizi mbili. Washiriki wa  mkutano huo walipendekeza mpango wa pamoja ili kupambana na wahalifu, pia uimarishaji wa uchunguzi wa mipaka pande zote mbili.

Lakini kile hasa kinachotakiwa na wakaazi wa huko ni viongozi kujitolea wenyewe binafsi kuirejesha amani mashariki mwa Kongo, kama alivyosisitiza Emmanuel Uvibo, mkaazi wa eneo la Aru huko Ituri. "Suala la usalama linatuhusu sisi sote. Tuna jukumu la kupiga kelele na kutoa wito kwa viongozi wetu kulishughulikia suala la Ituri kwa umakini. Tuna haki ya kumkumbusha rais kila wakati ili aweze kutupatia amani."

Upande mwengine, Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa hapa nchini, MONUSCO, kimetangaza mpango wa kuimarisha mbinu yake ya mapigano pamoja na jeshi la Kongo, dhidi ya vikundi vinavyomiliki silaha.
 

Symbolbild | DR Kongo | Anschlag der Alliierte Demokratische Kräfte Kongo
Picha: Alexis Huguet/AFP/Getty Images