1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali yazidi kuwa mbaya PAKISTAN.

6 Mei 2009

Hali inazidi kuwa mbaya, kaskazini magharibi mwa Pakistan huku wanajeshi wa serikali wakiendeleza mashambulizi dhidi ya Wataliban katika jimbo la SWAT.

https://p.dw.com/p/Hkdh
Wanajeshi wa Pakistan wanaendesha vita dhidi ya Taliban katika jimbo la SWAT.Picha: picture-alliance/ dpa

Maelfu ya watu wanasemekana wanaendelea kuyahama makaazi yao wakikwepa mashambulizi katika miji iliopo katika jimbo la SWAT. Rais Asif Zardari bila shaka ana mengi fikrani mwake akijitayarisha kukutana mara ya kwanza na Rais Barack Obama mjini Washington. Na katika nchi jirani ya Afghanistan shambulizi la wanajeshi wa Marekani limewaua watu 30.


Maelfu ya raia wakikimbia, milio ya makombora na silaha nzito ndizo picha ulimwengu unazishuhudia huku mapigano kati ya wanajeshi wa Pakistan na Wapiganaji wa kitaliban yakichacha katika jimbo la SWAT. kaskazini magharibi mwa Pakistan.


Mji wa Mingora, mji mkuu wa SWAT, ambao zamani ulikuwa kivutio kikubwa cha watalii sasa umeguezwa kuwa uwanja wa vita. Marufuku ya kutotaka nje iliyowekwa na serikali ya Pakistan haikuwashtua wataliban kwani wameipuuzilia mbali na wanaendelea kushika doria mjini humo.


Asif Ali Zardari
Rais Asif Zardari atakutana na Rais Obama leo, mjini Washington.Picha: pa / dpa

Vita hivi katika jimbo la SWAT viliingia katika daraja nyingine katika wiki mbili zilizopita- Pakistan ilikuwa inafuata mwito wa Marekani- Washington inaisukuma Pakistan iwazuie wataliban kuenea katika maeneo mengine nchini Pakistan. Yote haya yanatokana na Marekani kukerwa na serikali ya Asif Zardari kuwapa idhini Wataliban kuanzisha sheria ya dini ya kiislamu katika jimbo la SWAT.


Taliban waliposemekana kuingia katika mji wa Buner, uliopo kilomita 100 kutoka mji mkuu wa Islamabad, Marekani ikaanza kuisukuma Pakistan kuzima jaribio lolote la Taliban kufika Islamabad.


Kundi la Taliban limeshtumu mapiganao haya likisema serikali inakiuka makubaliano ya SWAT, msemaji wa Taliban, Muslim Khan anasema Pakistan ni kibaraka wa Marekani.


Ingawa rais Asif Zardari ametoa hakikisho kuwa Wataliban hawawezi kuipindua serikali yake, atakuwa na mengi ya kujibu katika mkutano wake wa kwanza na rais Barack Obama leo mjini Washington. Marekani imekerwa na jinsi serikali ya Pakistan imekuwa ikijivuta katika swala la kukabiliana na Wataliban- Marekani inadai Wataliban wana nia ya kuipindua serikali ya Pakistan- taifa linalomiliki silaha za nuklia.

Waziri wa usalama wa ndani wa Pakistan Rehman Malik anasema Pakistan iko imara.

Hamid Karzai PK in Kabul
Rais Hamid Karzai, wa Afghanistan pia atakutana na Obama.Picha: AP

Na katika nchi jirani ya Afghanistan, shambulizi la Marekani liliwaua watu 100. Marekani inasema ilikuwa inawalenga wapiganaji huko Afghanistan. Rais Hamid Karzai ambaye yupo mjini Washington kwa mazunguzo na rais Obama amesema hili ni swala bila shaka atatafuta jibu kutoka maafisa wa Marekani.


Mwandishi: Munira Muhammad/ afp

Mhariri: Aboubakary Liongo