1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali yazidi makali nchini Guinee

Oummilkheir13 Februari 2007

Waguinee hawana ruhusa ya kutoka zaidi ya saa nne kwa siku

https://p.dw.com/p/CHKK


Rais Lansana Konte wa Guinee ametangaza sheria ya hali ya hatari nchini humo.Watu wasiopungua tisaa wameuwawa kufuatia machafuko kati ya vikosi vya usalama na waandamanaji wanaolalamika dhidi ya kuchaguliwa waziri mkuu anaetajikana kuelemea zaidi upande wa rais.

„Uharibifu na hasara ya maisha ya binaadam ni kubwa mno kwa namna ambayo nimeamua kutangaza sheria ya hali ya hatari kote nchini“-amesema hayo rais Lansana Conté kupitia Radio ya taifa.

„Wakuu wa kijeshi wamepewa amri ya kufanya kila liwezekanalo kuwalinda raia dhidi ya hatari ya kuzuka vita vya wenyewe kwa wenyewe.“

Hali ya hatari inamaanisha sheria kali ya kutotoka nje,huku jeshi likiruhusiwa kumkamata yeyote anaetishia usalama wa taifa.

Mikutano ya hadhara imepigwa marufuku na jeshi limepewa amri ya kuzuwia magazeti yasichapishwe na vituo vya Radio na televisheni visitangaze.

Jeshi limepewa pia amri ya kusikiliza mawasiliano ya simu,kunasa Fax za watu na hata kukamata barua za watu.

Wakaazi wa Guinee wanaruhusiwa kutoka kati ya saa kumi za jioni hadi saa mbili za usiku tuu.

Vyama vya wafanyakazi vimeanza upya kugoma ijumaa iliyopita baada ya waziri Eugene Camara kuteuliwa kua waziri mkuu.

Vyama hivyo vinahoji kuteuliwa kwake ni kinyume na makubaliano ya kugawana madaraka yaliyofikiwa mwezi uliopita baada ya mgomo wa siku 18 uliogharimu maisha ya zaidi ya watu 90.

Jana vijana waliobeba marungu waliteremka majiani kufanya fujo katika miji mikuu kadhaa ya nchi hiyo.

Shughuli za kuchimba maadini ya Bauxite-yanayoipatia fedha za kigeni nchi hiyo ambayo uchumi wake umeporomoka licha ya utajiri wa mali asili ya kila aina-nazo pia zinaathirika kutokana na wimbi la machafuko ambalo kwa mujibu wa mashahidi limegharimu maisha ya watu watatu zaidi-wakati wa machafuko kati ya vikosi vya usalama na waandamanaji pembezoni mwa mji mkuu Conakry.

Maiti sita na majeruhi dazeni kadhaa,wamehesabiwa N’ZEREKORÈ mji wa pili mkuu wa Guinee,unaopakana na Liberia.

“Waandamanaji wametia moto nyumba ya Gavana”-amesema hayo meya wa mji huo Cece Loua mbele ya shirika la habari la Uengereza Reuters.

Hata migodi imeporwa-mashahidi wanasema.

Milio ya risasi imesikika karibu na uwanja wa ndege wa Conacry ambako hakuna hata ndege moja ya kutoka nje iliyotuwa tangu jumamosi iliyopita.

Wanajeshi wa kikosi cha ulinzi wa rais wamekivamia kituo cha matangazo RADIO FM LIBERTE na kuvunja vunja studio-baada ya msikilizaji wa radio hiyo kutoa mwito rais Conte ajiuzulu.