1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Harakati za kufufua mazungumzo ya Mashariki ya Kati

18 Machi 2010

Bibi Clinton, yupo Moscow na Ashton,Israel.

https://p.dw.com/p/MVn0
Hillary Rodham ClintonPicha: AP

Masaa 24 kabla ya mkutano wa kesho wa pande 4 zinazo ishughulisha na ufumbuzi wa mgogoro wa Mashariki ya Kati-Marekani,Urusi,Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya, waziri wa nje wa Marekani, Bibi Hillary Clinton, amewasili leo mjini Moscow .

Katika mazungumzo yake huko, mbali na kuondoa vikwazo vinavyozuwia kutiwa saini Mkataba mpya wa kupunguza boma la silaha za nuklia kati ya Marekani na Urusi,ziara yake ya masaa 36 itahusika pia na jinsi ya kuyakwamua mazungumzo yalionasa kati ya Israel na wapalestina.Mjumbe wa Marekani kwa Mashariki ya kati Bw.John Mitchel, alieahirisha ziara yake ya hivi punde, anatazamiwa kurejea Mashariki ya kati Ijumapili hii- kwa muujibu wa duru za Israel.

MJUMBE WA ULAYA ASHTON

Mbali na kuwasili Moscow, kwa waziri wa nje wa Marekani, mjumbe wa siasa za nje wa Umoja wa Ulaya,bibi Catherine Ashton, alikutana jana na waziri-mkuu wa Israel Benjamin Natanyahu pamoja na waziri wa nje Lieberman.Bibi Ashton, leo anakutana na viongozi wa Palestina kabla kesho kuwakilisha Umoja wa Ulaya katika mkutano wa pande 4 mjini Moscow.

Alipokuwa mjini Cairo juzi ambako alikutana na waziri wa nje wa Misri, Aboul Gheit na Jumuiya ya nchi za kiarabu-Arab League, Bibi Ashton alinukuliwa kusema,

"Natumai ijumaa utakachokiona ni pande 4 zilizopata ari na kasi mpya kushirikiana pamoja kuungamkono juhudi za amani ili zisonga mbele."

MRADI NYUMBA WA ISRAEL

Mipango iliotangaza Israel kujenga maskani mapya 1.600 ya walowezi wa kiyahudi katika Jeruselem ya mashariki waliokalia kijeshi,inazuwia kuanzishwa tena kwa mazungumzo ya amani kati yao na wapalestina-hayo alisema bibi Ashton mjini Cairo.

Wapalestina ambao karibuni hivi waliridhia kujiunga na mazungumzo ya amani yasio ya moja kwa moja na Israel ,wameapa kutorejea mezani kwa mazungumzo hayo hadi kwanza Israel, imefuta mpango wake huo wa kujenga majumba mengine 1.600 katika ardhi za wapalestina.

RAIS OBAMA

Nae Rais Barack Obama wa Marekani, alisema jana kuwa, mipango hiyo ya Israel ya kujenga majumba zaidi kandoni mwa Jeruselem ya mashariki , haisaidii juhudi za amani za mashariki ya Kati.Hatahivyo, alisema mada hii haikuzusha msukosuko katika usuhuba wa Marekani na mshirika wake wa chanda na pete.

TANGAZO LA ISRAEL NI MATUSI:

Waziri wa nje wa Marekani bibi Clinton nae alilieleza tangazo la ujenzi wa majumba hayo lililotolewa na Israel wakati makamo-rais wa Marekani, Joe Biden, akizuru Israel, wiki iliopita ni matusi. Bibi Clinton akatoa madai kadhaa ambayo alimtaka waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, kuhusu mradi huo wa majumba kuyatimiza na pia abainishe nia yake ya dhati kwa mazungumzo ya amani yasio ya moja kwa moja na wapalestina ambayo yaliafikiwa kufanywa wiki iliopita .

Msemaji wa wizara ya nje ya bibi Clinton,P.J Crowley,aliwaambia maripota kuwa, waziri mkuu Netanyahu bado hakumpigia simu Bibi Clinton kumpa majibu yake kabla mjumbe wake maalumu George Mitchell hakurejea Mashariki ya Kati ambako taarifa za Israel zadai angerejea Ijumapili hii ijayo.

Mwandishi: Ramadhan Ali / RTRE

Uhariri: Abdul-Rahman