1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Harakati za walinzi wa amani Jamhuri ya Afrika ya Kati

Sudi Mnette
30 Mei 2018

Miezi sita iliopita Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa likubali kupeleka wanajeshi 900 wa ziada Jamhuri ya Afrika Kati, kuimarisha moja wapo ya shughuli za kulinda katika taifa lenye mazingira hatari zaidi duniani.

https://p.dw.com/p/2yboo
Zentralafrikanische Republik  Bangui - Camp Kassaï Camp Kassaï
Picha: DW/H. Marboua

Hadi sasa ni wanajeshi 400 waliokwisha wasili, ikiwa ni ishara yenye kutia wasiwasi ya matatizo ambayo ujumbe wa Umoja huo unaojulikana kwa kifupi kwa lugha ya Kifaransa kama MINUSCA unakabiliana nayo katika kuzishawishi nchi wanachama kuchangia wanajeshi kwa jukumu hilo.

Duru za Umoja wa Mataifa zimesema, Brazil, Canada, Colombia, Cote d´Ivoire na Uruguay ni miongoni mwa nchi zilizoombwa kutoa wanajeshi lakini bila ya mafanikio yoyote. Hatimaye Nepal ilikubali kupeleka wanajeshi 600 na Rwanda na nchi nyengine zikakubali kupeleka wanajeshi 300. Duru hizo zimesema wanajeshi wote hao wanatarajiwa kuwa Bangui kabla ya muda wa shughuli hizo za Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Afrika Kati haujarefushwa mwezi Desemba.

Safari ya ulinzi  wa amani ya tangu 2014

Ujumbe  wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa umekuweko nchini humo tangu Aprili 2014, ukiwa na jukumu la kurejesha hali ya utulivu na utengamano nchini humo, baada ya  mgogoro wa kikatili wa kidini baina ya wanamgambo wa Seleka ambao wengi wao ni Waislamu na Anti-Balaka ambao ni Wakristo- mapigano ambayo Ufaransa ilijitahidi kuyazima. Ufaransa mkoloni wa zamani , ina wanajeshi 11,000 na polisi 2,000. Lakini wachambuzi wanahoji ikiwa ujumbe huo wa Umoja wa mataifa unaweza kupata mafanikio makubwa, kutokana na matatizo ambayo Jamhuri ya Afrika Kati inakabiliana nayo. Nchi hiyo iko katika hali ya mparaganyiko na sehemu kubwa ya maeneo yangali mikononi mwa wanamgambo wanaohasimiana, wengi wakidai wanazilinda jamii za Wakristo au Waislamu.

Kama zilivyo shughuli nyingi za kulinda amani za Umoja wa Mataifa kwengineko, kuna udhaifu mkubwa panapohusika na Jamhuri ya Afrika Kati. Kwa sehemu kubwa wanajeshi wa Umoja wa Mataifa hawatoshi na pia wana uhaba wa vifaa. Hayo yalifafanuliwa pia katika ripoti ya Shirika la Kimataifa linalohusika na migogoro-International Crisis Group mwaka jana 2017.

Kumbukumbu kubwa ya umwagikaji damu

Zentralafrikanische Republik christlicher Kämpfer
Mpiganaji wa kundi la Anti-BalakaPicha: picture alliance/AP Photo/J. Delay

Mnamo Aprili 9 na 10, mji mkuu Bangui ulishuhudia umwagaji mkubwa kabisa wa damu katika Kipindi cha miaka miwili iliopita, wakati watu 27 walipouwawa na zaidi ya 100 kujeruhiwa katika mapigano kati ya wanajeshi wa kulinda amani na wanamgambo katika eneo la Waislamu mjini humo. Wakaazi wa Kiislamu waliwatuhumu wanajeshi wa Umoja wa Mataifa kwa vifo vya watu 17, wakati jeshi hilo lilisema mapigano yalitokea baada ya wao kushambuliwa ghafla, wakiwa kwenye zoezi la kupiga doria. Mnamo Mei mosi, machafuko ya kidini yakasambaa baada ya watu waliokuwa na silaha kulivamia Kanisa, katikati ya misa na kuwauwa waumini na mhubiri.

Tokea ujumbe wa Umoja wa Mataifa kuanza kazi katika Jamhuri ya Afrika kati, imepoteza watu 73, watatu miongoni mwao tangu uanze mwaka huu 2018. Pia ujumbe wa Umoja wa Mataifa umekumbwa na malalamiko juu ya ukosefu wa nidhamu miongoni mwa wanajeshi wake pamoja na madai ya visa vya ngono na ukiukaji wa haki za binaadamu dhidi ya raia. Wanajeshi hao katika Jamhuri ya Afrika kati wanahusishwa na takriban theluthi moja ya madai yote ya visa vya ngono yalivyoripotiwa katika shughuli zote 15 za  kulinda amani duniani katika mwaka 2017. Kutokana na madai hayo, mnamo mwezi Machi Gabon iliamua kuwaondoa wanajeshi wake wote 444. Majadiliano yanaendelea kuitaka ibatilishe uamuzi huo na sasa hatua hiyo iliokuwa ianze kutekelezwa mwezi Juni imeahirishwa hadi Septemba. Wakati wa ziara yake mjini Bangui mwezo Oktoba mwaka jana, katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres aliliambia Shirika la Habari la AFP  wanaungama kuna matatizo hayo na kwamba watafanya kila wawezalo kuyashughulikia masuala hayo muhimu.

Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman, afp

Mhariri: Grace Patricia Kabogo