1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hasara ya kiuchumi na uharibifu wa misitu

H.Böhme/P.Martin30 Mei 2008

Mkutano wa uhai anuai wa Umoja wa Mataifa mjini Bonn,Ujerumani unamalizika leo hii.Kiasi ya wajumbe 6,000 kutoka nchi 190 wanashauriana njia ya kuzuia uteketezaji wa misitu na bahari pamoja na mimea na viumbe.

https://p.dw.com/p/E9y1
Bundesumweltminister Sigmar Gabriel, links, spricht am Montag, 19. Mai 2008 in Bonn auf der UN Konferenz zur Biologischen Vielfalt, die dort bis zum 30. Mai 2008 mit rund 5.000 Deligierten aus 170 Laendern stattfindet. (AP Photo/Hermann J. Knippertz) --- German Environment Minister Sigmar Gabriel, left, delivers a speech at the UN Conference on Biological Diversity in Bonn, Germany, on Monday, May 19, 2008. Some 5.000 delegates from 170 countries meet here until May 30, 2008. (AP Photo/Hermann J. Knippertz)
Waziri wa Mazingira wa Ujerumani Sigmar Gabriel(kushoto) akihotubia mkutano wa uhai anuai wa Umoja wa Mataifa mjini Bonn.Picha: AP

Waziri wa Mazingira wa Ujerumani Sigmar Gabriel,kama rais wa mkutano huo mjini Bonn,ametoa wito kwa mawaziri wenzake wa mazingira kukubaliana njia ya kukomesha kutoweka kwa mimea na viumbe mbali mbali hapa duniani.Amesema:

"Haya ni matukio yatakayokuja kuwaathiri watoto na wajukuu wetu katika siku zijazo.Hiyo ni sababu ya kuuliza:Kiuchumi,uhai anuai una thamani gani?Hasara gani ya kiuchumi inasababishwa na kutoweka kwa mimea na viumbe mbali mbali?"

Hayo ni baadhi ya masuala yaliyowashughulisha wajumbe usiku mzima kwenye mkutano wa Bonn.Wajumbe hao wamejigawa katika makundi mbali mbali kujadiliana njia ya kuhifadhi misitu,bahari,matumizi ya maliasili na hata mada ya utata kuhusu mafuta ya kuendeshea magari yanayotokana na mazao ya kilimo na jinsi uhai anuai yaani uhusiano wa mimea na viumbe kutegemeeana, unavyoathirika.

Siku ya Alkhamisi Waziri Gabriel aliashiria kuwa makubaliano,yalioitwa "Mwongozo wa Bonn" yamepatikana juu ya njia ya kugawana faida zinazopatikana kutokana na mimea na viumbe mbali mbali.

Vile vile kama nchi 60 zimekubali kuunga mkono mradi wa mfuko wa kuhifadhi wanyama duniani-WWF kukomesha uharibifu wa misitu katika nchi za tropiki.Mada kuu iliyojadiliwa katika mkutano wa siku kumi na mbili imehusika na njia ya kuhifadhi misitu,ikitathminiwa kuwa asilimia 80 ya mimea na viumbe mbali mbali hukutikana misituni.

Siku ya Jumatano,Kansela wa Ujerumani Angela Merkel alipofungua majadiliano ya kisiasa kwenye mkutano huo alisema,Ujerumani kati ya mwaka 2009 na 2012 itatoa kiasi cha Euro milioni 500 kusaidia kuhifadhi misitu iliyo katika hatari ya kutoweka.Na kuanzia 2013 Euro milioni 500 zingine zitatolewa kila mwaka kusaidia mradi huo.

Huu ni mkutano wa tisa wa Umoja wa Mataifa kuhusu uhai anuai.Mkutano huo ulizinduliwa mwaka 1992 kwenye Mkutano wa Mazingira mjini Rio de Janeiro,Brazil.