1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hatima ya Bafana Bafana na Ufaransa leo katika Kombe la Dunia

22 Juni 2010

Mexico na Uruguay /Nigeria na K.Kusini / Argentina na Ugiriki.

https://p.dw.com/p/Nzrg
Siboniso Gaxa ,mlinzi wa Bafana bafana (2) atazima hujuma za wafaransa leo ?Picha: AP

Baada ya Spain, mabingwa wa ulaya jana usiku ikitamba na David Villa, kuipiga kumbo Hondurus kwa mabao 2:0,macho ya mashabiki hasa wa nyumbani Afrika Kusini , yanakodolewa mpambano wa alaasiri ya leo kati ya wenyeji-Bafana Bafana na Ufaransa-timu ambayo inaonekana kusambaaratika .Mpambano wapili ambao pia utaamua hatima ya Afrika Kusini na Ufaransa, ni ule unaochezwa sambamba kati ya Mexico na Uruguay.

Timu hizi mbili za Amerika ya kati na kusini, zinahitaji kutoka sare tu, ili kila moja ikate tiketi yake kwa duru ya pili.Kufanya hivyo, lakini , kunakumbusha kashfa ya Kombe la Dunia,1982 huko Spain, pale Ujerumani na Austria,zilipopanga matokeo na kuitoa mhanga Algeria.

Swali linaloulizwa na mashabiki wa Afrika Kusini na Afrika nzima, ni Je: Leo mazumari ya "vuvuzela" yatahanikiza kwa mara ya mwisho au la.Afrika Kusini, lazima iishinde Ufaransa na kutumai Mexico na Uruguay, zinafungana. Ama sihivyo, Kombe la Dunia 2010 ,la kwanza barani Afrika, litamalizika kabla ya wakati na sio tu kwa Bafana Bafana, bali hata kwa Ghana,yenye miadi kesho na Ujerumani katika mpambano wa kufa-kupona kwa kila moja.

PARREIRA ANA TURUFU GANI ?

Kocha wa Bafana bafana,mbrazil Carlos Parreira,ameahidi kufanya mabadiliko 5 katika kikosi kilichozabwa mabao 3-0 na mabingwa wa kwanza kabisa wa dunia-Uruguay.

Kumekuwapo pia mfarakano katika kikosi hicho cha Bafana Bafana.Wachezaji wa mkoa wa Kwazulu-Natal, yasemekana hawakufurahishwa na kutocheza kwa ari kwa wenzao kutoka klaubu za Johannesberg na Pretoria. Hatahivyo, mazumari ya mashabiki wa Bafana bafana, yatazamiwa kuhanikiza leo alao kwa mara ya mwisho. Kocha Parreira amesma kwamba, wanawaheeshimu wafaransa lakini, hawawaogopi.Ufaransa, iliilaza Afrika kusini 3:0 katika Kombe la Dunia, 1998 huko Ufaransa.

UFARANSA NA HATIMA YAKE ?

Ufaransa,makamo bingwa wa dunia 2006 na mabingwa nyumbani, 1998 waliaibishwa na walipochapwa mabao 2:0 na Mexico.Hii ilitanguliwa na sare ya 0:0 na Uruguay. Kocha wa kutatanisha wa Ufaransa, Raymond Domenech, ameungama aliposema, " Sasa, tunnahitaji miujiza kusonga mbele."

Kampeni ya makamo-bingwa hawa wa dunia, ilikumbwa na msukosuko baada ya wachezaji wa kikosi cha Les B lue,walipogoma kufanya mazowezi ili kulalamika kwa kutimuliwa mwenzao ,mshambulizi wa Chelsea, Nicolas Anelka.

Cha kuangalia leo pia, mbali na mpambano kati ya Ufaransa na Afrika kusini mjini Bloemfontein, ni vipi Uruguay na Mexico, zitakavyocheza.Je, zitatoka sare huko Rustenburg ? Itakua kashfa nyengine ? Moja ni wazi,ili wasonge mbele, tangu wafaransa hata Bafana bafana, watapaswa kuigiza Ureno ilivyocheza jana na kutia mabao mengi.

Leo usiku, itakua zamu ya Nigeria kucheza mpambano wake wa mwisho na Korea ya Kusini, kabla kuwafuata Simba wa nyika Kameroun,nyumbani.Nigeria, haina pointi wakati Korea ya kusini, ina pointi 3. Sambamba na mpambano huo, Argentina, inayopigiwa upatu kuvaa tena taji la dunia kama Brazil,inamaliza duru hii na Ugiriki.

Mwandishi : Ramadhan Ali /AFPE

Uhariri: Abdul-Rahman