1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hatima ya Hosni Mubarak magazetini nchini Ujerumani

Oumilkher Hamidou7 Februari 2011

Eti Mubarak aachiwe kuja kuishi Ujerumani,akitimuliwa nchini Misri?Wahariri hawana msimamo mmoja kuhusu suala hilo

https://p.dw.com/p/10BzO
Waandamanaji mjini CairoPicha: picture-alliance/dpa

Tunaanza na gazeti la Südkurier linalozungumzia vuta nkuvute kati ya Mubarak na waandamanaji.Gazeti linaendelea kuandika:

Kwa wakati wote ambao Mubarak atajifungia ndani ya kasri lake,maandamano ya kila siku ya umma na machafuko yataendelea mjini Cairo.Hali hiyo inakorofisha suluhu na kuzidi kuyatia hatarini maisha ya binaadam.Kwa hivyo lingekua jambo la busara kama serikali kuu ya Ujerumani ingepiga moyo konde na kumruhusu mwanasiasa huyo mkongwe wa miaka 82 aje Ujerumani kwa kisingizio cha matibabu.Alipokuwa kipenzi cha magharibi,Mubarak aliwahi kukaribishwa Ujerumani kwa matibabu.Lakini anaemkaribisha muimla aliyeshindwa anabidi ataambue kwamba milele hawezi Mubarak kusalia humu nchini.Sasa atapelekwa wapi baadae?Arejeshwe Misri?Na famailia yake ?Na akonti zake zilizoko nchi za nje?Kwa wakati wote ambao masuala kama haya hayatopatiwa majibu,Ujerumani haiwezi kuwa mahala pa kukaribishwa mzee huyo.

Gazeti la "Badische Neueste Nachrichten linajiuliza:

Tathmini na hoja za wale wanaojiita wataalam zinazidi kumiminika kuhusu Misri.Kana kwamba walijua au angalao waliashiria kinachotokea.Abadan.Au kulikuwa na angalao mmoja aliyewahi miezi ya nyuma kuzungumzia uwezekano wa kuzuka machafuko nchini Tunisia au kuripotiwa magazetini jinsi watu wanavyoteswa na utawala wa Mubarak?

Ägypten Unruhen in Kairo Panzer
Vifaru katika uwanja wa TahrirPicha: dapd

"Der neue Tag linajaribu kuleta uwiano kati ya yaliyotokea Iraq na upepo wa mabadiliko ulioanzia Tunisia na kuandika:

Mashariki ya kati upepo hauvumi kama rais wa zamani wa Marekani George W.Bush na washirika wake katika uvamizi wa Iraq wa mwaka 2003 walivyokuwa wakitarajia.Sio kutoka nchi ya mito miwili,bali nchi ndogo ya Tunisia ndiko upepo wa mageuzi ulikoanzia na kulitikisa eneo zima.Mapambano ya kuania uhuru yamewaingia waatunisia,wayemen,wa-Jordan na wa-Misri bila ya msaada wa nchi za magharibi.Irak haikuchukuliwa kama mfano wa kuigizwa kama Bush alivyoahidi,kinyume kabisa inaangaliwa kama mfano wa mfarakano na umwagaji damu.Waandamanaji hawakutegemea chochote kutoka nchi za magharibi seuze kutoka Marekani.

Na hatimae gazeti la Süddeutsche Zeitung linaandika:

Utawala wa Mubarak umedhoofika.Lakini bado upo madarakani.Ni vyema kwamba rais anasema amechoka-viongozi wa chama tawala cha NDP wamejiuzulu-mtoto wa kiume wa Mubarak, aliyekuwa amrithi madarakani-Gamal,amezipa kisogo harakati za kisiasa.Lakini mfumo wa utawala haukutikisika.Makamo wa rais ni wa kutoka idara ya upelelezio , waziri mkuu mpya,ni jenerali wa zamani na waziri mpya wa mambo ya ndani pia.Jeshi linadhamini usalama:lakini si jeshi la wananchi ni vikosi vinavyomtii shujaa wa vita Mubarak.Kwa hivyo utawala wa kiimla hauongozwi na Mubarak peke yake.

Mwandishi:Hamidou Oummilkhheir/Inlandspresse

Mpitiaji:Abdul-Rahma Mohammed