1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hatima ya Kosovo yajadiliwa Umoja wa Mataifa

P.Martin2 Aprili 2007

Mpango unaopendekeza kuipa Kosovo uhuru wa kiwango fulani utakaosimamiwa,utajadiliwa upya na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa siku ya Jumanne.

https://p.dw.com/p/CHH1

Mpatanishi mkuu wa Umoja wa Mataifa,Martti Ahtisaari atahotubia Baraza la Usalama lenye wanachama 15,kueleza mapendekezo yake kuhusu Kosovo.Mapendekezo hayo yalitangazwa Jumatatu iliyopita,huku Belgrade na Moscow zikipinga vikali.Kikao hiki kitasikiliza tu maelezo ya mpango wa Ahtisaari ambao unaungwa mkono na Marekani na Umoja wa Ulaya.

Umoja wa Mataifa unaliongoza jimbo la Kosovo tangu katikati mwaka 1999,baada ya kumalizika kampeni ya shirika la kujihami la magharibi NATO. Kampeni hiyo ya mashambulio ya bomu,ilikomesha matumizi katili ya nguvu ya vikosi vya Serbia dhidi ya wakazi wa Kosovo ambao wengi wao ni wa asili ya Kialbania.Wakati wa mgogoro wa Kosovo,kati ya mwaka 1998 na 1999,kiasi ya watu 10,000 wenye asili ya Kialbania waliuawa na wengine kwa maelfu walilikimbia jimbo hilo.

Ahtisaari,katika ripoti yake amesema,uhuru ni njia pekee ya kuwa na Kosovo yenye utulivu wa kisiasa na kiuchumi.Lakini ameeleza waziwazi kuwa hapo mwanzoni,Kosovo iliyo huru itapaswa kusimamiwa na jumuiya ya kimataifa.Kuambatana na mpango huo,baada ya kutangazwa kwa hadhi mpya ya jimbo la Kosovo,katiba mpya yapaswa kuidhinishwa katika muda wa siku 120.Hapo,ndio yatamalizika mamlaka ya tume ya hivi sasa ya Umoja wa Mataifa. Vile vile,uchaguzi mkuu na chaguzi za serikali za mitaa zinapaswa kufanywa katika muda wa miezi 9 kufuatia hadhi mpya ya Kosovo.Mjumbe wa kiraia atakaekuwa mjumbe wa Umoja wa Ulaya ndio atasimamia utaratibu wa kutekelezwa mpango wa Ahtisaari.Mjumbe huyo lakini,hatohusika moja kwa moja na uongozi wa Kosovo.Usismamizi huo wa kimataifa utamalizika,pale Kosovo itakapotekeleza hatua zote zilizopangwa katika mpango uliopendekezwa na Ahtisaari.

Lakini Serbia inayoitazama Kosovo kama ni kitovu cha ustaarabu wake,inapinga vikali penedekezo la kuipa Kosovo uhuru wa aina fulani.Waziri mkuu wa Serbia,Vojislav Kostunica anatazamiwa kuhudhuria kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Hata Urussi iliyo mshirika mkuu wa Belgrade na ikiwa na kura ya turufu katika Baraza la Usalama, imeimarisha upinzani wake dhidi mpango wa Ahtisaari kuhusu hatima ya Kosovo.