1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hatimaye mbinyo wazidi kwa Theresa May kuondoka madarakani

Sekione Kitojo
23 Mei 2019

Waziri mkuu wa Uingereza Theresa  May anaendelea kulenga kukamilisha kujitoa nchi hiyo kutoka Umoja wa Ulaya yaani Brexit na  atakutana  na mawaziri, amesema msemaji wake, huku kukiwa na miito ya kutaka ajiuzulu.

https://p.dw.com/p/3Iyb5
Reportage London vor Europawahl 2019 Daily Mail Theresa May
Picha: DW/B. Wesel

Hayo ni baada  ya  mpango wake  wa hivi  karibuni  wa  Brexit kukosolewa  kwa  kiasi  kikubwa. 

Mswada wa sheria ya  kujitoa  kutoka Umoja wa Ulaya  wa  waziri mkuu  Theresa  May  uliondolewa  bila  kutarajiwa  kutoka  katika mpango wa  shughuli za serikali  bungeni  mapema  mwezi Juni, leo Alhamis, na  kuzusha tetesi  zaidi  kuhusu  hali  yake  ya  baadaye.

England Brexit Rede Premierministerin Theresa May
Waziri mkuu wa Uingereza Theresa MayPicha: Reuters/K. Wigglesworth

Serikali ya chama cha  Conservative  imekuwa  ikitarajia  kuweka msukumo  katika  mswada  wa  makubaliano  ya  kujitoa  hapo kesho  Ijumaa  katika  baraza  la  wawakilishi, la  wabunge  wa kuchaguliwa. Lakini  Mark Spencer, akikaimu  nafasi ya  kiongozi  wa bunge  hilo kutoka  chama  cha  May, Andrea Leadsom, ambaye alijiuzulu  jana, amesema  serikali  sasa  itachapisha  mswada baada  ya  bunge  kwenda  mapumziko kuanzia  Ijumaa  hadi  Juni 3.

Mbunge Mel Stride aliteuliwa  kuwa  kiongozi  wa  serikali  bungeni katika  baraza la  wawakilishi  leo, akichukua  nafasi ya  Andrea Leadsom ambaye  amejiuzulu  akipinga  mkakati  wa  waziri  mkuu May  katika  Brexit.

Shughuli za serikali bungeni

Stride  ambaye, hapo  kabla  alikuwa  naibu waziri katika  wizara  ya  fedha, atachukua  jukumu  hilo la uwandamizi  ambalo linabeba  wajibu  wa  kuendesha  shughuli  za serikali  bungeni.

Waziri mkuu May yumo katika  mbinyo wa kutaka  ajiuzulu  baada ya juhudi  zake  za  mwisho  za  Brexit  kugonga  mwamba na  amekubali kukutana  na  mwenyekiti wa  chama chake  cha  Conservative kesho Ijumaa kujadili juu  ya  hatma yake. Kuna idadi  kadhaa  ya viongozi wa  chama  cha  Conservative  ambao wako  njiani kuwania  wadhifa  wa  waziri mkuu May.

Boris Johnson ambaye  alijiuzulu  kuwa  waziri wa  mambo  ya  kigeni mwezi Julai kuhusiana  na upinzani wake dhidi ya May alivyolishughulikia  suala  la majadiliano ya kujitoa nchi  yake  katika Umoja  wa  Ulaya ni  mmoja  kati ya wanaotarajiwa  kuwania  kiti cha Theresa May.

Guy Verhofstadt
Mbunge wa bunge la Ulaya Guy VerhofstadtPicha: picture-alliance/W. Dabkowski

Mbunge wa  bunge  la  Ulaya  Guy Verhofstadt  amesema  leo kwamba  kura ya  maoni  iliyopigwa  Uingereza  kujitoa  kutoka Umoja  wa  ulaya , ilikuwa  ni  maafa  kwa  Ulaya , lakini  imekuwa na  athari  kwamba  hakuna  mtu  mwingine  katika  bara  hilo anataka  kuona  nchi  nyingine  ikijitoa  kutoka  Umoja  huo.