1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hatimaye rais wa Algeria Abdelaziz Bouteflika ajiuuzulu

Amina Mjahid
3 Aprili 2019

Rais Abdelaziz Bouteflika wa Algeria amekabidhi barua yake ya kujiuzulu akiachia madaraka wakati kukiwa na maandamano makubwa dhidi yake baada ya miongo miwili ya uongozi wake.

https://p.dw.com/p/3G98U
Algerien, Algier:  Algerisches Militär fordert Absetzung von Präsident Bouteflika
Picha: picture alliance/dpa

Sauti za honi za magari zilisikika mijini Algiers kabla ya watu waliobeba na kupeperusha bendera za Algeria kutoka majumbani mwao na kumiminika mitaani wakishangiria habari ya kujiuzulu kwa rais Abdelaziz Bouteflika.

Kulingana na televisheni ya kitaifa nchini humo, Bouteflika aliliambia rasmi baraza la katiba juu ya hatua ya kumaliza muda wake uongozini,kama rais wa Jamhuri ya taifa hilo la Afrika ya Kaskazini.

Algerien Protest gegen Präsident Abdelaziz Bouteflika in Algiers
Picha: picture-alliance/abaca/L. Ammi

Barua ya kujiuzulu kwake ilioonekana na shirika la habari la serikali APS, imemnukuu Bouteflika akisema hatua aliyoichukua anatumai itatoa nafasi kwa Algeria kusonga mbele na kuwa na mustakabali mwema.

Algeria kwa sasa inapitia kipindi cha mpito baada ya rais huyo kujiuzulu, na masualai juu ya nini kitafuata kwa taifa hili tajiri kwa gesi na mshirika wa Magharibi katika kupambana na Ugaidi yameanza kuibuka.

Baraza la kikatiba lililo na wanachama 12 nchini humo linatarajiwa kukutana  hii leo kuthibitisha hatua ya kujiuzulu kwa Bouteflika. Kituo cha televisheni ya taifa  hata hivyo kilimuonesha kiongozi huyo anaeugua akimkabidhi rasmi barua yake ya kujiuzulu rais wa baraza hilo Tayeb Belaiz.

Baraza la Katiba kukutana na kuthibitisha hatua ya Bouteflika ya kujiuzulu

Katiba ya Algeria inasema rais akifariki dunia au kujiuzulu baraza la katiba ni lazima lithibitishe, kabla ya mabunge yote mawili kukutana na spika wa bunge kuteuliwa kama rais wa mpito kwa siku 90, wakati uchaguzi wa rais ukiandaliwa. Kwa hiyo moja kwa moja Abdelkader Bensalah aliye na miaka 77 mshirika wa Bouteflika ambaye ndiye spika wa bunge la sasa nchini Algeria ndiye rais wa mpito.

Tayeb Belaiz
Picha: DW

Marekani kwa upande wake imepongeza hatua ya Abdelaziz Bouteflika kujiuzulu na kusema mustakabali wa waalgeria kwa sasa utaamuliwa na wa Algeria wemyewe. Robert Palladino msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani amesema masuala juu ya namna mipango yote itakavyoeendeshwa baada ya Bouteflika kujiuzulu itaamuliwa na wwatu wa taifa hilo.

Naye Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian amesema hatua ya rais Bouteflika inafungua ukurasa mpya na muhimu katika historia ya Algeria.

Rais huyo wa zamani wa Algeria aliye na miaka 82 aliyeshutumiwa kwa muda mrefu kung'ang'ania madaraka, amekumbana na shinikizo kubwa la kumtaka ajiuzulu baada ya hatua yake ya kutaka kuwania muhula wa tano madarakani licha ya kutoonekana hadharani baada ya kuugua kiharusi mwaka 2013.

Mwandishi:  Amina Abubakar/AFP/AP/Reuters

Mhariri: Yusuf Saumu