1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hatimaye ripoti ya CAG Assad yaingia bungeni Tanzania

Mohammed Khelef
10 Aprili 2019

Katika hali isiyotegemewa, bunge nchini Tanzania limeiweka ripoti ya mdhidhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali, CAG Mussa Assad, kwenye orodha ya shughuli zake, licha ya kuazimia kutoshirikiana naye.

https://p.dw.com/p/3GY3U
Tansania Daressalam Präsident John Magufuli
Picha: DW/E. Boniphace

Katika hali isiyotegemewa, bunge nchini Tanzania limeiweka ripoti ya mdhidhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali, CAG Mussa Assad, kwenye orodha ya shughuli zake, licha ya kuazimia kutoshirikiana naye.

Mapema siku ya Jumatano (Aprili 10), orodha ya shughuli za bunge ilionesha kuwa ripoti hiyo muhimu kwa shughuli za udhibiti wa kodi za wananchi ingeliwasilishwa bungeni hapo, na muda mchache baadaye ofisi ya mkaguzi huyo ikatoa taarifa ya kukutana na waandishi wa habari kwenye ofisi zake na sio ofisi za bunge kama ilivyokuwa huko nyuma.

Kwenye mkutano wake na waandishi wa habari, CAG Assad alisema waliamuwa kufanyia mkutano wao huo mahala hapo kwa kuwa walishahofia kuwa huenda wasingealikwa bungeni. Hata hivyo, kwa mujibu wa mkaguzi huyo, waliwaalika wabunge na wenyeviti wa kamati za bunge, ingawa hawakuhudhuria mkutano huo. 

Kuhusu ukaguzi wao kwa mwaka wa kifedha uliomalizika Juni 2018, uligunduwa kuwa jumla ya kodi ya shilingi bilioni 119 haikukusanywa kutoka kwa walipakodi, huku Shirika la Bima la Taifa likinunuwa mfumo wa dola milioni 3.59 ambao haufanyi kazi hadi sasa. 

Aliwaambia waandishi wa habari pia kwamba mashirika 14 ya umma, likiwemo la ndege - ambalo limekuwa moja ya alama za mafanikio ya utawala wa Rais John Magufuli - yana matatizo makubwa ya kifedha yanayopelekea kuwa na madeni mengi zaidi kuliko mitaji yake.

Tansania Wahl des Premierministers Kassim Majaliwa
Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai.Picha: DW/H. Bihoga

Kuhusu vyama vya siasa

Miongoni mwa mapungufu yaliyotajwa na Profesa Assad kwenye mkutano wake na waandishi wa habari ni matumizi na malipo yasiyo na maelezo ya kuridhisha kutoka vyama vikubwa vya kisiasa, kikiwemo kinachotawala (CCM) na chama kikuu cha upinzani (CHADEMA) sambamba na vyama vyengine kama vile CUF.

Kwa upande wa CCM, ukaguzi umebaini kuwa chama hicho hakijawasilisha makato ya shilingi bilioni 3.74 ya wanachama wake kwa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) huku kwa upande wa Zanzibar kikimiliki nyumba zaidi ya 100 kwa majina ya wanachama na sio bodi ya wadhamini kama inavyotakiwa. 

Hali kama hiyo pia imebainika kwa chama cha CUF, ambacho baadhi ya majengo yake yameandikishwa kwa majina ya watu, huku CHADEMA wakibainika kununuwa gari lenye thamani ya dola 63,000 kwa jina la mtu binafsi.

Kuhusu neno udhaifu

Kuhusu utata wa neno 'udhaifu' ambalo ndilo hasa lililosababisha maamuzi ya bunge ya kutofanya kazi naye, Profesa Assad alisema kuwa ofisi yake ingelindelea kulitumia kama kawaida kwani linamaanisha kile hasa kilichogunduliwa na ukaguzi wao na ni lugha ya kawaida kwenye taaluma yao.

Mtaalamu huyo wa ukaguzi ambaye ameingia kwenye mzozo na bunge linaloongozwa na Spika Job Ndugai, alisema kuwa katika ukaguzi wao wa mwisho walitoa jumla ya mapendekezo 350 ya kufanyiwa kazi, lakini hadi sasa ni 80 tu yaliyoshughulikiwa.

Kuwasilishwa kwa ripoti hii bungeni kunachukuliwa na wanaharakati na wapinzani nchini humo kama ushindi wa wazi kwao kwa kile wanachosema ni uwajibikaji wa mamlaka husika. 

Awali, wanaharakati wanaojiita Mabadiliko Tanzania waliwasilisha barua yenye sahihi zaidi ya 15,000 za wananchi kushinikiza bunge kuipokea na kuifanyia kazi ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali, baada ya siku kuzidi kuyoyoma bila kuwasilishwa bungeni na ofisi ya rais.