1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hatma ya kesi ya Kenyatta na Ruto kujulikana leo

15 Novemba 2013

Umoja wa Afrika unalitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, leo kupiga kura kuahirisha kwa mwaka mmoja kesi ya uhalifu wa kibinaadamu dhidi ya viongozi wa Kenya katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ya ICC.

https://p.dw.com/p/1AI9d
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta na makamu wake William Ruto
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta na makamu wake William RutoPicha: Simon Maina/AFP/Getty Images

Wanadiplomasia wanasema kuwa rasimu ya azimio hilo linalotaka kuahirishwa kwa kesi inayomkabili Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya na makamu wake, William Ruto, linaonekana kushindwa kutokana na kutoungwa mkono kwa kiasi kikubwa. Ni wanachama saba tu kati ya 15 wa baraza hilo, ndiyo wanaliunga mkono azimio hilo.

Ili liweze kupitishwa, azimio hilo linahitaji kupigiwa kura na wanachama tisa, lakini hata hivyo, linaweza kupingwa kwa kupigiwa kura ya turufu na mataifa kama vile Uingereza na Ufaransa, yanayoiunga mkono kwa kiasi kikubwa Mahakama ya ICC, iliyoko The Hague. Marekani bado haijajiunga na mahakama hiyo kupitia mkataba wa Roma, lakini inaunga mkono malengo yake.

Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC, Fatou Bensouda
Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC, Fatou BensoudaPicha: AFP/Getty Images

Umoja wa Afrika unasema kwamba kuahirishwa kwa kesi hiyo, kutaipa Kenya muda wa kuimarisha usalama wake katika kukabiliana na vitendo vya kigaidi, baada ya mashambulizi ya kigaidi ya mwezi Septemba mwaka huu.

Shinikizo lilitokana na shambulizi la kigaidi

Shinikizo la kuahirishwa kwa kesi hiyo limeongezeka baada ya kutokea mashambulizi hayo ya kigaidi yaliyosababisha mauaji ya watu 67 na wengine kadhaa kujeruhiwa. Hata hivyo, wanadiplomasia wa mataifa ya Magharibi na wanaharakati wanaiona hatua hiyo kama kampeni ya kisiasa.

Mahakama ya ICC imewafungulia Kenyatta na Ruto mashtaka ya uhalifu dhidi ya ubinaadamu kwa kuhusika kwao na ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka 2007, ambazo zilisababisha zaidi ya watu 1,000 kuuawa. Kenyatta anashtakiwa kwa ubakaji na vitendo vingine vya ukatili vilivyofanywa na kundi la kihalifu linalojulikana kama Mungiki, ambalo linadaiwa lilikuwa chini yake.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki MoonPicha: Reuters

Kenyatta aliyechaguliwa kuwa rais wa Kenya mwanzoni mwa mwaka huu, amesisitiza kuwa hana hatia, kama ilivyokuwa kwa makamu wake, William Ruto, ambaye kesi yake tayari imeanza kusikilizwa.

Ama kwa upande mwingine, kura ya maoni iliyoendeshwa nchini Kenya, imeonyesha kuwa asilimia 67 ya Wakenya wanataka Rais Kenyatta ahudhurie kesi dhidi yake huko ICC, ili akajibu shutuma zinazomkabili. Utafiti huo uliofanywa na shirika la Ipsos Synovate, unaonyesha kuwa asilimia hiyo ya raia 2,060 wa Kenya walioulizwa, waliona ni bora Rais Uhuru aende ICC kujibu kesi dhidi yake.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/APE,AFPE
Mhariri: Josephat Charo