1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hatma ya muungano wa CDU/CSU yaning'inia

Saumu Mwasimba
2 Julai 2018

Kansela Merkel akutana na kiongozi wa CSU Horst Seehofer kujadiliana zaidi kuhusu suala la wakimbizi linaloibua mvutano kati ya washirika wakuu wa kisiasa.Mkutano wa Berlin utaamua hatma ya muungano

https://p.dw.com/p/30gaG
Deutschland | Merkel trifft Seehofer im Kanzleramt
Picha: picture-alliance/dpa/P. Zinken

 Kansela Angela Merkel na Kiongozi wa chama cha Christian Social Union CSU Horst Seehofer wanakutana mjini Berlin leo (02.07.2018) kutafuta mwafaka juu ya mvutano kuhusu sera ya wakimbizi.Mkutano baina ya viongozi hao wanaovutana kuhusu sera ya wahamiaji unatajwa kwamba utasimamiwa na spika wa bunge la Ujerumani Wolfgang Schaeuble. Mkutano huu unatarajiwa kuamua juu ya hatma ya serikali ya muungano ya Ujerumani.

Kansela Angela Merkel ameanzisha juhudi za mwisho za kujaribu kumshawishi waziri wake wa mambo ya ndani Horst Seehofer baada ya waziri huyo kutishia kujiuzulu kutokana na Merkel kuendelea kushikilia msimamo wa kukataa hatua kali za kudhibiti mipaka zilizopendekezwa na kiongozi huyo wa chama cha Christian Social Union CSU cha jimbo la Bavaria. Viongozi wa CDU na wenzao wa CSU wanajadiliana jioni hii kutafuta njia za kufikia maridhiano lakini ikiwa hakuna kitakachokubaliwa muungano wa vyama hivyo ndugu CSU na CDU huenda ukavunjika,na kitakachofuatia ni uwezekano wa serikali ya Kansela Merkel inayoundwa na vyama vitatu kuanguka. Jumapili(01.07.2018) Kiongozi wa CSU Horst Seehofer alisema

Horst Seehofer, Angela Merkel
Picha: picture alliance/dpa/P.Kneffel

"Nimeshauambia mkutano kila kitu.Na kwa mara nyingine kesho yaani leo tutakuwa na mazungumzo zaidi kujaribu kupata makubaliano kuhusu suala muhimu la kudhibiti mipaka na kuwarudisha wakimbizi kwa maslahi ya nchi yetu na kwa uwezo wa  muungano wa kuchukua hatua  kwa maslahi ya serikali  ambayo tunataka kuiendeleza. Nataraji tutafanikiwa. Hii ni hatua ya nia njema kwa upande wangu kutoa nafasi nyingine ya kujaribu.Vinginevyo huu uamuzi wa leo  ndio ungekuwa wa mwisho.

Seehorfer ameonesha kwamba huenda akawa tayari kuendelea kuwa waziri wa mambo ya ndani ikiwa chama cha CDU kitaridhia hatua ya kuwarudisha walikotoka wakimbizi waliosajiliwa katika nchi nyingine za Ulaya wanaofika katika mipaka ya Ujerumani kutaka hifadhi. Waziri wa uchumi Peter Almaier ambaye ni mshirika wa karibu wa Merkel anasema kwamba wamefanya kila wawezalo kuondowa tafauti zao na wataendelea kufanya kila wanachoweza  kuhakikisha muungano wa CDU na CSU unabakia.Hata hivyo kupizia ujumbe wa Twitta waziri wa zamani wa mambo ya nje kutoka SPD Sigmar Gabriel amesema Seehofer ameiteka nyara Ujerumani nzima pamoja na Umoja wa Ulaya.Kwa upande mwingine waziri wa ajira kutoka chama hicho cha SPD Hubert Heil anasema.

''Kinachoendelea ndani ya CDU na CSU na hasa ndani ya CSU ni kitu kinachosababisha wasiwasi SPD.Tunachoweza kufanya ni kuwatolea mwito kwamba,hapa suala sio kuhusu maslahi ya waliowachache bali ni kuhusu jinsi tunavyoipeleka nchi.

Deutschland Berlin Andrea Nahles, SPD-Vorsitzende zu Unionskrise
Picha: picture-alliance/dpa/B.v. Jutrczenka

Chama cha Kijani na SPD kinachounda serikali pamoja na Muungano  wa vyama ndugu CDU na CSU vinasema vimejiandaa kwa matokeo yoyote ya mkutano wa leo ikiwemo suala la uchaguzi mpya.Kiongozi wa chama cha SPD Andrea Nahles ameitisha pia mkutano wa kilele wa dharura utakaofanyika baade leo Jumatatu kati ya vyama hivyo vinavyounda serikali CDU,CSU na Spd.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri:Josephat Charo