1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hatua ya kijeshi yavuka kiunzi cha kwanza

5 Septemba 2013

Ombi la Rais Barack Obama la kutaka bunge la Marekani liunge mkono kwa haraka shambulio la kijeshi dhidi ya Syria limepiga hatua katika kamati ya baraza la Seneti baada ya kuungwa mkono hapo Jumatano (04.09.2013).

https://p.dw.com/p/19cRv
Maafisa waandamizi wa serikali ya Marekani wakiwasilisha hoja ya kuchukuliwa hatua ya kijeshi katika kamati ya seneti.
Maafisa waandamizi wa serikali ya Marekani wakiwasilisha hoja ya kuchukuliwa hatua ya kijeshi katika kamati ya seneti.Picha: Reuters

Ombi hilo limepitishwa saa chache baada ya rais kuweka wazi uwezekano wa kuamuru kuchukuliwa kwa hatua hiyo kufuatia shambulio la silaha za sumu lililosababisha maafa nchini Syria hata kama bunge la nchi hiyo halitoridhia kuchukuliwa kwa hatua hiyo.

Azimio lenye kuunga mkono matumizi ya nguvu dhidi ya serikali ya Rais Bashar al Assad limevuka kiunzi cha kamati ya mambo ya nje ya baraza la Seneti hapo jana kwa kura 10 -7. baada ya kuimarishwa dakika za mwisho kwa kujumuisha ahadi ya kufanya mabadiliko muhimu kwenye uwiano wa kijeshi uliopo hivi sasa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria ambapo vikosi vya Marekani havitopelekwa nchini humo kwenye mapambano.Azimio hilo litafikishwa kwenye baraza la seneti lenyewe wiki ijayo juu ya kwamba wakati wa kulipigia kura bado haujulikani.

Kuungwa mkono kulikoonekana kwenye baraza la seneti hakutokuwa rahisi kupatikana kwenye baraza la wawakilishi ambalo linadhibitiwa na wabunge wa chama cha upinzani cha Republikan ambalo pia linalitafakari ombi hilo la Obama juu ya kwamba ratiba yake ya kulipigia kura haijulikani kabisa.

Assad ametumia silaha za sumu

Mjini Washington waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry na maafisa wengine waandamizi wa serikali waliwasilisha hoja za kutaka kuchukuliwa kwa hatua hiyo ya kijeshi katika kikao cha kwanza cha baraza hilo la bunge la Marekani kufuatia ombi la Obama la kutaka kibali cha bunge kuishambulia Syria.

Kerry amesema Assad ametumia silaha za kemikali mara 11,likiwemo moja katika majira ya chipukizi ambapo wakati huo Obama hakuwa na ushahidi wa kutosha kushinikiza kuchukuliwa hatua hiyo ya kijeshi.Kerry amesema "Dunia inajiuliza iwapo Marekani itaridhia shambulio hilo la silaha za sumu kwa njia ya kubaki kimya,kukaa pembeni wakati unyama huo ukiachiliwa kutokea bila ya kuchukuwa hatua ya kuuwajibisha."

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry akitetea hoja ya hatua ya kijeshi dhidi ya Syria katika kamati ya Seneti.
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry akitetea hoja ya hatua ya kijeshi dhidi ya Syria katika kamati ya Seneti.Picha: Reuters

Alipoulizwa juu ya kuungwa mkono kimataifa jua ya hatua hiyo ya kijeshi Kerry amesema jumuiya ya Nchi za Kiarabu imekubali kulipia gharama ya hatua yoyote ya kijeshi itakayochukuliwa na Marekani,hakufafanuwa kima kitakachotolewa ingawa ameseme ni kikubwa mno.

Suluhisho la amani

Kwa upande wa pili Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amesema hapo Jumatano kwamba licha ya kupunguwa kwa matarajio ya kupatikana kwa ufumbuzi wa amani kwa mzozo huo wa Syria atapigiganis juhudi za kufikia suluhisho katika mkutano wa leo wa kundi la G20 unaofanyika St.Peterburg Urusi. Amesema hata kama hakuna matumaini hayo lazima mtu aendelee kujaribu na hivyo ndivyo anavyoiona dhima yake katika mzozo huo.

Kauli yake hiyo inakuja wakati waziri wake wa ulinzi Thomas de Maiziere akisema kwamba ni jambo lililo wazi kwamba vikosi vilivyo tiifu kwa serikali ya Bashar al-Assad vilitumia gesi ya sumu dhidi ya raia.De Maziere amesema kumekuwepo na mfululizo wa ushahidi unaonyesha kwamba hilo linawezekana na kwamba kwa maoni yake ushahidi huo hautowi nafasi ya kuwekewa mashaka. De Maziere amekiambia kituo cha utangazaji cha MDR Info kwamba "Kila kitu anachokisikia kinaashiria kwamba hilo lilikuwa shambulio lililofanywa na serikali na Bw. Assad anawajibika na hilo."

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Thomas de Maiziere.
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Thomas de Maiziere.Picha: picture-alliance/dpa

De Maziere amesema ni muhimu kusubiri repoti kutoka kwa wataalamu wa Umoja wa Mataifa ili kwamba umma wa dunia ujulishwe " sio tu kutoka mashirika ya ujasusi ya mataifa ya magharibi bali pia wakaguzi wa Umoja wa Mataifa ambao wanaaminika sana ."

Mwandishi: Mohamed Dahman/Reuters/AFP/AP

Mhariri: Mohammed Khelef