1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hatua ya makundi yafikia kikomo

Bruce Amani
4 Desemba 2017

Hatua ya makundi ya Champions League inakamilika wiki hii, wakati vilabu kadhaa vikitafuta tikiti ya kujiunga timu nane ambazo tayari zilitinga katika hatua ya mchujo

https://p.dw.com/p/2ojHm
München Pressekonferenz Jupp Heynckes
Picha: picture-alliance/dpa/M. Balk

Katika Kundi A, viongozi Manchester United wanawaalika kesho CSKA Moscow, ambao wako katika nafasi ya pili pamoja na Basel. United wanahitaji tu pointi moja tu ili kuongoza kundi hilo

Manchester City wanasafiri kuchuana Jumatano na Shakhtar Donetsk wakiwa tayari wameshinda Kundi F na wenyeji hao watajiunga nao, kama hawatashindwa na kisha Napoli nayo iishinde Feyenoord.

Katika Kundi E mambo ni magumu sana ambako Liverpool wanawaongoza Sevilla na Spartak Moscow, ambao watacheza Anfield Jumatano. Liverpool wanaweza kuongoza kundi hilo kama watashinda mechi ya Jumatano na wataweza kufuzu kama watatoka sare, lakini wanaweza pia kuondolewa kama watazabwa nao Sevilla washinde.

Chelsea wamefuzu na wanaweza kuongoza Kundi C kwa kupata ushindi dhidi ya Atletico Madrid au kama Roma hawatawazaba Qarabag. Atletico wanaweza kutupwa lakini watahitaji kushinda nao Roma wazabwe.

Juventus wanaweza kumaliza katika nafasi ya pili ya Kundi D kama watashinda Olympiacos. Hata kama watazabwa, watafuzu tu, kama Sporting Lisbon wataangushwa na Barcelona

Katika kundi G, Besiktas watacheza dhidi ya RB Leipzig, ijapokuwa wamefuzu kama washindi wa kundi hilo, na Porto watajiunga nao kama watashinda mechi yao dhidi ya Monaco

Kundi B litakamilika kwa mchuano kati ya Bayern Munich na PSG lakini wenyeji wanaweza kuwapiku PSG katika uongozi wa kundi hilo kama watawafunga Zaidi ya mabao manne.

Tottenham Hotspur wameshinda kundi H kabla ya kuwaalika Apoel Nicosia wakati Real Madrid wakiwa wa pili na watamaliza kazi dhidi ya Borussia Dortmund.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/AP/Reuters
Mhariri: Yusuf Saumu