1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hatua ya Trump ni hatari kwa dunia, pigo kwa Ulaya

Lilian Mtono
9 Mei 2018

Hisia na chuki za muda mrefu ambazo wengi walionesha katika ikulu ya Marekani, White House kuhusu makubaliano ya mpango wa nyuklia wa Iran huenda zilielezwa vizuri na aliyekuwa afisa msaidizi wa usalama Sebastian Gorka.

https://p.dw.com/p/2xQ2u
Deutsche Welle Michael Knigge
Picha: DW/P. Henriksen

Hisia na chuki za muda mrefu ambazo wengi walionesha katika ikulu ya Marekani, White House kuhusu makubaliano ya mpango wa nyuklia wa Iran huenda zilielezwa vizuri na aliyekuwa afisa msaidizi wa usalama Sebastian Gorka. Ufuatao ni uhariri wa mwandishi wa DW, Michael Knigge baada ya rais wa Marekani Donald Trump kuiondoa Marekani kwenye mkataba wa nyuklia wa Iran.

Matamshi makali aliyoyatoa siku ya Jumanne wakati akitangaza maamuzi ya kuiondoa Marekani kwenye mkataba huo, rais Donald Trump, alirudia matamshi yake ya muda mrefu kwamba mkataba wa Iran ni mbaya kwa Marekani na dunia, na hivyo washirika wa Marekani wakubaliane na tathmini hiyo.

Mkataba wa Iran uliifanya dunia kuwa salama zaidi.

Bila shaka mpango wa makubaliano wa Iran haukuwa bora na hakuna makubaliano ambayo huwa kamilifu, ila ni kile ambacho kiliafikiwa baada ya zaidi ya muongo wa mazungumzo ya kimataifa ya kuzuia mpango wa nyuklia wa Iran kwa kipindi cha muda mfupi na wa kati.

Iran imeendelea kukubaliana na matakwa ya mkataba huo, ukweli ambao umekuwa ukithibitishwa na wachunguzi huru wa kimataifa na maafisa wa usalama wa Marekani, na kwa ujumla ulikubalika duniani kote, licha ya madai yaliyoibuliwa hivi karibuni na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, ambayo pia yalirejelewa na Trump hapo jana.

Iran Parlament Protest gegen US-Austieg aus dem Atomabkommen
Iran imesema itaendelea kusalia kwenye mkataba huo, hata bila ya MarekaniPicha: picture-alliance/AP Photo

Mkataba huo ulifikiwa kupitia ushirikiano ambao mara kwa mara ulikuwa mgumu lakini wa karibu zaidi kati ya Marekani na Ulaya, ulioongozwa na kile kilichoitwa E3, yaani Ujerumani, Ufaransa na Uingereza. Ni muhimu pia kutambua kwamba China, Urusi na kwa ujumla jumuiya ya kimataifa pia waliuunga mkono. Lakini zaidi, mkataba huo wa nyuklia pia ulitoa mwelekeo wa namna ya kukabiliana na mipango ya nyuklia kwa amani na mafanikio na wahusika wasumbufu wa kimataifa.

Washirika wa Ulaya hawajakubaliana.

Dhana isiyo sahihi kwamba washirika wa Marekani wana mtazamo sawa na rais wa Marekani kuhusu mkataba wa Iran ni madai mepesi kuyatoa baada ya kansela Angela Merkel wa Ujerumani, na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ambao hivi karibuni walizuru ikulu ya White House, kama hatua za mwisho mwisho za kumshawishi Trump kutoachana na mkataba huo wa nyuklia. Kwa hakika, ni sawa na kofi la uso kwa Ulaya ambao wamekuwa wakiupigania kwa ukweli na uaminifu. Na hata kwa Israel, viongozi wa kijeshi mara kadhaa wameeleza kuwa wangependelea Marekani isalie kwenye mkataba huo.

Siasa za ndani ndizo huamua sera za kigeni.

Bila ya kukosea, hatua ya Trump ya kuiondoa Marekani kwenye mkataba huo ina machache ya kuchangia katika mkakati wa kimataifa ambao huenda ungeifanya dunia kuwa salama zaidi ama kuongeza maslahi ya Marekani na washirika wake, lakini ina mengi ya kufanya na hisia za wapiga kura na siasa za ndani.

USA Trump verlässt den Raum ARCHIV
Trump anakabiliwa na lawama kutoka sehemu mbalimbali kutokana na hatua yake hiyo.Picha: picture-alliance/NurPhoto/C. May

Trump na wengi wa wafuasi wake na wasaidizi wake wameamua kudharau kila ambacho kilifanywa na mtangulizi wake Barack Obama, na wamefanikisha azma yao ya kufuta urithi wake, na hasa kwa mkataba huu wa nyuklia wa Iran, ambao ni alama ya mafanikio makubwa ya sera ya nje ya Obama, tangu alipowabadilisha mshauri wa zamani wa usalama wa taifa H.R McMaster na waziri wa mambo ya nje Rex Tillerson, aliyetetea Marekani ibakie kwenye mkataba huo, na John Bolton na Mike Pompeo wanaoupinga vikali.   

Makubaliano mapya?
Nini kitafuata baada tangazo la Trump la kujiondoa kwenye mkataba wa nyuklia wa Iran bado si dhahiri, kwa kuwa hakuna matayarisho yoyote mbadala yaliyowekwa wazi, zaidi ya ahadi jumla ya rais kwamba atafanya makubaliano ya mkataba bora zaidi. Hili bado ni swali kubwa, kwa kuwa kuna mwitikio mdogo wa makubaliano mapya kwa Ulaya na Iran lakini pia kwa Jumuiya ya kimataifa. 

Wasiwasi waongezeka kuhusu mazungumzo ya Korea Kaskazini.

Wakati hatua hiyo ya Trump ikizusha wasiwasi ni dhahiri kwamba kuachana na mkataba huo wa Iran kutaongeza tu shinikizo kubwa lililopo kuelekea mazungumzo ya rais Trump na kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un.

Shinikizo hilo sio kwa Kim, kama Trump anavyodhani na kudai, lakini kwa rais mwenyewe. Hii ni kwa sababu baada ya kujiondoa kwenye makubaliano ya kimataifa ambayo yalifanikisha kudhibiti mipango ya nyuklia ya Iran, Trump sasa anatakiwa kutoa mkataba ambao ni bora zaidi. Iran haikuwa na silaha za nyuklia, lakini Korea Kaskazini inazo.

Mwandishi: Knigge, Michael/Lilian Mtono
Mhariri:Josephat Charo