1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hatua za haraka kuchukuliwa kumaliza baa la njaa

Kabogo Grace Patricia16 Novemba 2009

Hayo yamo katika azimio la mwisho lililofikiwa kwenye mkutano wa masuala ya usalama wa chakula duniani.

https://p.dw.com/p/KYLh
Mkuu wa shirika la FAO, Jacques Diouf.Picha: AP

Mkutano wa kilele wa masuala ya usalama wa chakula duniani umeahidi kuchua hatua za haraka kumaliza baa la njaa linalowaathiri zaidi ya watu bilioni moja duniani kote. Ahadi hiyo imo katika azimio la mwisho lililofikiwa hii leo Jumatatu katika mkutano huo unaofanyika mjini Roma, Italia.

Marais na wakuu wa serikali wapatao 60 kutoka karibu mataifa 200 duniani wanahudhuria mkutano huo wa siku tatu uliopewa jina ''Mkutano wa Njaa'' unaofanyika katika makao makuu ya Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa-FAO. Mashirika ya kibinaadamu yamekosoa jinsi ambavyo viongozi wa nchi tajiri duniani hawajahudhuria mkutano huo na kulishutumu azimio hilo lililofikiwa kwa kuondoa kipengele cha Umoja wa Mataifa kinachotaka kumalizwa kabisa baa la njaa duniani ifikapo mwaka 2025.

Welternährungsgipfel 2009 in Rom
Wajumbe mkutanoni.Picha: AP

Ahadi za mkutano wa Julai mjini L'Aquila

Katika mkutano wa kundi la mataifa tajiri duniani-G8 uliofanyika mwezi Julai mwaka huu mjini L'Aquila, Italia, nchi hizo ziliahidi kutoa dola bilioni 20 kwa ajili ya shughuli za kilimo katika kipindi cha miaka mitatu ijayo lakini hadi sasa hakuna kilichofanyika na ahadi hiyo imebakia kuwa hadithi. Msemaji wa shirika la Oxfam, Frederic Mousseau amesema mataifa tajiri duniani hayaonyeshi shauku ya kumaliza tatizo hilo na pia hawaoni uharaka wake. Mkuu wa shirika la FAO, Jacques Diof amependekeza dola bilioni 44 zitolewe kila mwaka kwa ajili ya kusimamia shughuli za maendeleo katika sekta ya kilimo.

Akizungumza kuhusu hali ya njaa ilivyo duniani Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Mazingira-UNEP, Achim Steiner amesema,''Ni watu wachache wanaotambua kwamba wakati tunakabiliwa na matatizo ya usalama wa chakula duniani na pia upungufu wa chakula kutokana na ongezeko la idadi ya watu duniani,kwa upande mwingine ni wazi kwamba mifumo ya uzalishaji na uuzaji bidhaa za kilimo unapoteza kiasi cha asilimia 30 hadi 40 ya kila kinacholimwa.''

Katibu Mkuu Ban na Papa Benedikto XVI

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon katika mkutano huo amesema makubaliano ya kupunguza gesi zinazoharibu mazingira mwezi ujao mjini Copenhagen, Denmark, ni muhimu katika kukabiliana na baa la njaa duniani kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa kuwaumiza zaidi wakulima katika nchi masikini. Bwana Ban amesema hapawezi kuwa na usalama wa chakula bila ya kuwa na usalama wa hali ya hewa.

Kwa upande wake, kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Baba Mtakatifu Benedikto wa Kumi na Sita akizungumza katika mkutano huo amesema utajiri na uharibifu wa mali havina nafasi katika dunia ambayo njaa inaongezeka. Baba Mtakatifu ametoa wito wa kuwepo uwezekano wa masoko ya kimataifa kuingiza bidhaa kutoka nchi masikini ambazo anasema mara nyingi zimekuwa zikiwekwa kando.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (RTRE/AFPE/APE)

Mhariri: M.Abdul-Rahman