1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hertha Berlin yailaza B.Munich 2:1

16 Februari 2009

Berlin yaparamia kileleni mwa Bundesliga.

https://p.dw.com/p/GvRU
Andrey Voronin atia bao. **Picha: AP

Bayern Munich,mabingwa wa Ujerumani, watimuliwa kileleni mwa Bundesliga na Hertha Berlin baada ya kukomewa mabao 2-1.Manchester United na Everton, zimeingia robo-finali ya Kombe la FA-Raul avunja rekodi ya mabao mengi ya Di Stefano-stadi mashuhuri wa Real Madrid na Uwanja wa Taifa wa Tanzania uliojengwa kwa msaada wsa China, umefunguiliwa rasmi jana mjini Dar-es-salaam.

Katika medani ya riadha,bingwa wa zamani wa rekodi ya dunia ya mita 100 Asafa Powell wa Jamaica ,ataongoza mabingwa kadhaa wa olimpik wa Beijing katika mashindano ya riadha mjini Sydney na Melbourne,Australia.

Ligi mashuhuri barani Ulaya:

Hertha Berlin, timu ya jiji kuu la Ujerumani, imeparamia kileleni mwa Bundesliga mwishoni mwa wiki baada ya kuwachezesha mabingwa Bayern Munich kindumbwe-ndumbwe na kuwalaza kwa mabao 2:1. Andrey Voronin,alipiga kwanza hodi katika lango la Bayern Munich tayari katika kipindi cha kwanza na kukaribishwa ndani.

Miroslav klose, hakukawia kusawazisha kwa B.Munich,lakini Voronin,akapiga tena hodi na kwa mara ya pili akaitikiwa na kwa bao hilo la pili,Munich iliotazamia kunyakua usukani wa Bundesliga kutoka chipukizi Hoffenheim,waliolazwa mabao 4-1 na Bayer Leverkuisen, ilijikuta inaangukia nafasi ya 4 nyuma ya Hamburg katika ngazi ya ligi. Hertha Berlin ,inaongoza sasa Bundesliga ikiwa na pointi 40,wakifuatwa nyuma na Hoffenheim yenye pointi 39 sawa na Hamburg,walioilaza jana Armenia Bielefeld mabao 2-0.

Kocha wa Hamburg mwishoe, alisema:

"Kikawaida uklicheza kama tulivyocheza leo,huhitaji kutetemeka ukitiwa bao 1.Nimefurahi kuona tumerudi kileleni na sio kama ilivyokuwa wiki iliopita tulipotoa pointi sadaka."

Nae kocha wa Hertha Berlin,viongozi wapya wa Bundesliga alisema:

"Mambo mwiashoe yameenda uzuri kabisa mbele ya mashabiki wetu 75,000.

tumeishinda Bayern Munich kwa mabao 2:1 na hii yatosha kwa leo."

Borussia Moenchenglasdbach, inaburura bado mkia wa Ligi kwa pointi zake 13 na pamoja na Cottbus na karlłsruhe, zenye pointi 17 kila moja iko hatarini kuweza kurudi daraja ya pili.

Ligi ya Uingereza -Premier League, kwa kadiri kubwa ilipumzika mwishoni mwa wiki na kutoa nafasi kwa Kombe la FA-Kombe la shirikisho la la dimba la Uingereza:

Manchester United na Everton, ni miongoni mwa timu 8 zilizokata tiketi zao za robo-finali ya kombe hilo la FA.Manu iliitandika Derby County mabao 4-1 wakati Everton iliitimua nje Aston Villa kwa mabao 3-1.Nani alikuwa wa kwanza kuipatia Manu bao pale alipolifumania lango la Derby County kwa mkwaju mkali katika dakika ya 28 ya kipindi cha kwanza kabla Gibson kutia bao la pili kufuatia mkwaju mkali wa freekick aliouchapa Cristiano Ronaldo .Ronaldo akatia binafsi bao la 3 kwa kichwa kabla Addison hakurejesha bao 1 kwa Derby.

Katika La Liga-Ligi ya Spain, Raul jana aliaandika historia alipoivunja rekodi ya stadi wa Argentina alieichezea Real Madrid- Di Stefano ya jumla ya mabao 307. Raul alitia bao katika lango la Gijon kuipa ushindi Real wa bao 4:0 na kuivunja rekodi ya Di Stefano.Lilikuwa bao lake la 309 .Raul ambae ameongoza Rewal madrid kutwaa ubingwa mara 3 ameweka rekodi mpya.

Raul ameichezea Real Madrid muda mrefu zaidi kuliko Di Stefano.Stadi wa Argentina-di Stefano, alitia jumla ya mabao 307 kwa Real kati ya 1953 na 1964 na aliisaidia Real kutawazwa mara 6 mabingwa wa ulaya kwa mabao yake.

Raul alieisaidia Real kutwaa ubingwa wa Spain mara 3 ameivunja rekodi ya Di Stefano ,ameanza kuichezea Real madrid tangu 1994.

Katika changamoto za La Liga mwishoni mwa wiki-viongozi wa Ligi FC Barcelona walimudu sare ya mabao 2:2 na Sevilla wakati Valencia iliondoka pia sare ya bao 1:1 na Malaga.Jana Real Madrid iliikomea Sporting Gijon kwa mabao 4:0 huku Racing Santander ikitoka suluhu ya bao 1:1 na Villareal.

Rais wa Jamhuri ya Watu wa China,Hu Jintao akiwa pamoja na rais Jakaya Kikwete wa Tanzania,aliufungua rasmi Uwanja wa Taifa wa dimba jana mjini Dar-es-salaam .Rais wa China alitimiza hapo ombi la Rais Benjamin Mkapa alipozuru Beijing akifuatana na rais wa sasa wakati ule akiwa waziri wa nje.Uwanja huo unakisiwa ni miongoni mwa ya kisasa kanda ya Afrika mashariki na kati.

Riadha: Bingwa wa zamani wa rekodi ya dunia ya mita 100,mjamaica Asafa Powell ataongoza kundi la wanariadha wa kasi katika changamoto za mwaka huu za mjini Sydney na Melbourne,Australia.

Powell ataungana na na Muamerika Xavier carter na bingwa wa medali ya fedha wa michezo ya Olimpik ya Beijing kwa masafa ya mita 400 kuruka viunzi Melaine Walker pia kutoka Jamaica.

Bingwa wa dunia wa mita 400 kuruka viunzi kutoka Marekani na bingwa wa medali ya dhahabu wa Jumuiya ya madola Van Zyl kutoka Afrika Kusini watashiriki pia katika mbio hizo za kuruka viunzi.

Serikali ya New Zealand yamkini ikaamrisha timu yake ya Taifa ya Cricket kutokwenda Zimbabwe kwa ziara iliopangwa hapo Julai.hii amearifu waziri mkuu John Key leo.Baraza la mawaziri la NZ bado halikuzingatia swali hilo,lakini hadhani kuwa timu ya NZ itakwenda Zimbabwe. New Zealand hapo itafuata mfano wa waziri mkuu wa zamani wa Australia John Howard alieizuwia timu ya cricket ya Australia kutembelea Zimbabwe 2007.