1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hicks afikishwa mahakamani Guantanamo

P.Martin26 Machi 2007

Muaustralia David Hicks hii leo anafikishwa mbele ya Mahakama mpya ya kijeshi iliyoundwa na Marekani hivi karibuni.Hicks anatuhumiwa kuwa alipigania mtandao wa kigaidi wa Al-Qaeda nchini Afghanistan na kwa njia hiyo ameunga mkono ugaidi wa kimataifa.

https://p.dw.com/p/CHHX
Picha ya Hicks mahakamani
Picha ya Hicks mahakamaniPicha: AP

David Hicks ni miongoni mwa wafungwa wa kwanza kabisa kupelekwa Guantanamo Bay.Yeye alikamatwa Afghanistan mwaka 2001 na mapema mwaka 2002 alisafirishwa hadi Kuba kwenye jela ya jeshi la Marekani.Hicks mwenye umri wa miaka 32 vile vile ni wa kwanza kati ya hao wanaoitwa wapiganaji haramu walio maadui,kufikishwa mahakamani Guantanamo baada ya kuzuiliwa kwa muda wa miaka mitano.Afisa wa habari katika jela ya Guantanamo Bay Captain Bruce Roberts amesema kuwa serikali ina ushahidi dhidi yao na imefungua mashtaka kwa sababu inaamini imekusanya ushahidi wa kutosha kwamba watuhumiwa hao wamefanya vitendo vinavyokwenda kinyume na sheria za kijeshi au dhidi ya Mkataba wa Geneva na kwa hivyo wanashtakiwa uhalifu wa kivita.

Kwa kweli Mahakama ya Kijeshi ilitazamia kusikiliza kesi za washtakiwa hao tangu mwaka mmoja uliopita,baada ya jengo hilo kujengwa kwenye uwanja wa ndege wa zamani wa kituo cha jeshi la Marekani huko Guantanamo.Jengo hilo lilibakia tupu tangu Mahakama Kuu ya Marekani mjini Washington kupitisha uamuzi wake mwaka jana kuwa kesi hizo zinakwenda kinyume ya katiba.

Kwa maoni ya Charles Swift aliekwenda hadi Mahakam Kuu ya Marekani kumtetea Salim Ahmed Hamdan aliekuwa dreva wa Bin Laden na kushinda kesi yake,Korti ya Kijeshi inaitishwa kwa sababu moja tu yaani ili isishindwe kesi.Anauliza kwanini basi kuwa na kesi?Kwani kila mmoja anafahamu kuwa hiyo si cho chote isipokuwa ni hadaa ya kisiasa.

Swift sasa ametoka jeshini na bado ni mkosoaji mkubwa wa serikali ya Bush na anasema,tangu mwanzoni jela ya Guantanamo Bay ilifunguliwa ili sheria za Marekani zisiweze kutumika huko. Itakumbukwa kuwa mwaka jana,wakati chama cha Bush cha Republikan kilidhibiti bunge,mahakama ya kijeshi iliidhinishwa na bunge hilo.Hatua hiyo iliwashtusha wanasheria na wapigania haki za binadamu.Sababu mojawapo ni kuwa mahakama hiyo huruhusu ushahidi wa watu wasiotajwa majina na ule unaopatikana kwa mateso.Kwa mfano,David Hicks amesema kuwa ameteswa mara nyingi.Hata Muingereza Shafik Rasul ambae sasa ameachiliwa huru amesema walifungwa chini na minyororo kwa saa nyingi katika hali ya maumivu ili watamke kuwa ni wanachama wa Al-Qaeda.Anasema hatimae walikubali tu ili maumivu yapate kusita.

Adhabu kali kabisa ni kifo lakini David Hicks hatokabiliwa na adhabu hiyo kwani mashtaka mengine yameondoshwa na sasa anashtakiwa kusaidia shirika la kigaidi.Kwa mujibu wa wakili wake, Hicks atasema kuwa yeye hana hatia.