1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hiddink awapa onyo wachezaji wa Chelsea

24 Desemba 2015

Kocha mpya wa Chelsea Guus Hiddink, amewataka wachezaji wake kuwa makini na kuzingatia uwepo wao katika timu hiyo ili kusaidia kuyaimarisha matokeo yao.

https://p.dw.com/p/1HSdw
Guus Hiddink
Picha: imago/VI Images

Hiddink alipewa wiki iliyopita wadhifa huo hadi mwishoni mwa msimu huu, kuchukua mikoba ya Jose Mourinho ambaye alionyeshwa mlango kufuatia matokeo mabaya ya timu.

Chelsea, mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Kandanda England hadi sasa wanashikilia nafasi ya 15 kwenye msimamo wa ligi, baada ya kucheza Mechi 17.

Mholanzi Hiddink amesema kwa kupiga hesabu, The Blues wanaweza kumaliza katika nafasi ya nne msimu huu ili wacheze katika dimba la UEFA Champions League msimu ujao lakini ni kazi ngumu.

Hii ni mara ya pili kwa Hiddink kupewa jukumu la ukufunzi uwanjani Stamford Bridge ambapo mara ya kwanza ilikuwa katika msimu wa 2008/09 alipotimuliwa Luiz Felipe Scolari. Wakati huo aliiongoza Chelsea kwa kipindi cha miezi mitatu ya mwisho na kuwasaidia kunyakuwa Kombe la FA, wakafika nusu fainali ya Champions League na kumaliza Nafasi ya tatu kwenye Ligi ya Premier pointi saba nyuma ya mabingwa Manchester United.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Mohamed Khelef