1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hiddink kuchukua nafasi ya Mourinho

18 Desemba 2015

Guus Hiddink, anajiandaa kuchukua usukani kama kaimu kocha wa Chelsea hadi mwisho wa msimu, kujaza pengo lililoachwa na Jose Mourinho aliyepigwa kalamu siku ya Alhamisi

https://p.dw.com/p/1HQ5K
Guus Hiddink
Picha: picture-alliance/dpa

Hiddink yuko mjini London ambako amekuwa akifanya mazungumzo na uongozi wa Chelsea.

Mholanzi Hiddink, mwenye umri wa miaka 69, alitekeleza jukumu sawa na hilo mnamo mwaka wa 2009, wakati alipoteuliwa baada ya Luiz Felipe Scolari kutimuliwa, na akaiongoza Chelsea kutwaa kombe la FA.

Kumekuwa na mchanganyiko wa hisia na maoni kuhusiana na hatua ya kutimuliwa Jose, miongoni mwa mashabiki wa kandanda. Wengi wamehisi ni uamuzi mzuri huku wengine wakipinga huku wakiwalaumu wachezaji kwa kile wanasema ni kumhujumu kocha wao.

Aliyekuwa kocha wa Chelsea Ray Wilkins anasema Hiddink anatosha kabisa kujaza nafasi hiyo ili kuiokoa Chelsea ambayo inayumba baada ya mwanzo mbaya msimu huu.

Sasa kuna maswali mengi yanaoulizwa, baada ya Hiddink kuchukua kama kaimu kocha, nani atapewa kazi hiyo katika mkataba wa kudumu? Kuna majina ambayo yanazungumziwa, wakiwemo, Carlo Ancelotti ambaye kwa sasa hana mkataba baada ya kuachishwa kazi na Real Madrid, Diego Simeone, kocha wa Atletico Madrid, Antonio Conte, kocha wa timu ya taifa ya Italia, miongoni mwa wengine.

Na jee, Jose Mourinho sasa atakwenda wapi baada ya Chelsea?

Mreno huyo mwenye umri wa miaka 52 amepata mafanikio makubwa katika kazi yake, kando na Chelsea, alifunza na kushinda mataji akiwa na Porto, Inter Milan na Real Madrid.

Miongoni mwa timu ambazo huenda The Special One anaweza kujiunga nazo ni kama vile, Manchester United, Bayern Munich, au hata mabingwa wa Ufaransa Paris Saint Germain.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri: Yusuf Saumu